Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Waitara akizindua ukumbi wa chakula wa shule ya msingi Mlimwa iliyopo Area C mjini Dodoma. Ukumbi huo wenye thamani ya shilingi milioni 81.5 umejengwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali liitwalo CDTF kwa kushirikiana na kanisa la KKKT.
**************
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Mwita Mwikwabe Waitara (MB) amesema kuwa serikali haijakataza michango shuleni isipokuwa ile iliyokuwa ya lazima na akataka michango hiyo ifuate mwongozo wa serikali wa kuchangia.
Akizindua jengo jipya la bwalo la chakula lililojengwa na shirika lisilo la kiserikali la CDTF jana katika shule ya msingi mlimwa iliyopo katikati ya jiji la Dodoma, Mhe.Waitara amesema kuwa wapo watu wamekuwa wakipita pita huko mitaani na kutoa tafsiri potofu kuwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano amepiga marufuku michango yote shuleni jambo ambalo si la kweli.
Amesema kuwa michango ambayo Mhe.Rais aliyokataza ni ile ya lazima ambayo ilikuwa ikilazimisha watoto wote shuleni kuchangia ama wana uwezo au la jambo lililokuwa likisababisha watoto wanaokosa kulipia michango hiyo kutokana na wazazi au walezi wao kukosa fedha hufukuzwa shule.
“Ila nafahamu kuwa yapo baadhi ya maeneo ambapo watu wamepotosha, tunao waraka wa serikali wa mwaka 2016, unaoelekeza ni aina gani ya michango inayopaswa kutolewa, namna gani michango ifanywe, na kina nani wasimamie, “ amesema na kuongeza:
“ waraka umeeleza kuanzia mtu wa kawaida hadi ngazi ya taifa, na umeelezwa vizuri kabisa, lakini watu wenye nia zao mbaya walifanya kusudi kabisa kupotosha wazazi wasichangie,” amesema.
Mhe. Waitara ameongeza kuwa maelekezo ya serikali ni kwamba walimu washirikiane na kamati za shule, na viongozi wa serikali, wakae pamoja wajadiliane namna ya kuchangia ili wale wazazi au walezi ambao wana uwezo wa kuchangia wachangie lakini wale wasio na uwezo wasichangishwe na pia wahakikishe watoto wanaotoka familia masikini wasiondolewe madarasani kwa wazazi wao kushindwa kutoa michango.
Akizungumzia hafla hiyo ya kuzindua bwalo hilo la chakula, Mhe.Waitara amelipongeza shirika la CDTF, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania pamoja na uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha kuwa bwalo hilo linakamilika ili kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kupata chakula cha mchana shuleni.
Amesema kuwa ni muhimu kwa wazazi na walezi kutambua kuwa watoto wao wanapaswa kupatiwa chakula shuleni ili waweze kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri masomo yao.
Mhe. Waitara pia amewapongeza wazazi na walezi wa shule ya msingi Mlimwa A kwa kuitikia vizuri wito wa serikali kuhakikisha kuwa wanachangia maendeleo ya shule kwa kuwapatia uji kila siku watoto wote wanaosoma shule hiyo.
“Ndiyo maana katika taarifa ya Mwalimu Mkuu inaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo watoto wote wanaomaliza darasa la saba katika shule hii wameenda sekondari,”amesema.
Mhe.Waitara amesema watu wazima wanaposhiriki semina waandaaji huhakikisha kuwa washiriki wanapatiwa chai asubuhi, na mchana hupewa chakula, na akashangaa kwa nini watoto wanaosoma katika shule wasile chakula hivyo akawahimiza wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule zote nchini kuona umuhimu wa kuchangia ili watoto wao wapate chakula shuleni ili wasome kwa bidii na waweze kufaulu vizuri.
Mapema Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mlimwa Bi Salma Machaku alisema kuwa kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018 katika matokeo ya kumaliza darasa la saba katika shule hiyo ufaulu umekuwa wa asilimia 100, kadhalika pia kwa darasa la nne jambo ambalo alidai limechangiwa na uongozi mzuri wa shule hiyo.
Amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo lenye thamani ya shilingi 81, 592, 478 utawawezesha wanafunzi wa shule hiyo kupata chakula kwenye eneo salama, pia watumishi wataweza kuandaa chakula katika hali ya usafi, na pia ukumbi utaweza kuwaingizia kipato kupitia kuendesha mikutano mbalimbali ikiwemo ile ya shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CDTF Tanzania bwana Henry Mgingi amesema mradi huo wa ukumbi mbali na shilingi milioni 81 za wahisani, pia wazazi walichangia shilingi milioni 3 na halmashauri ya jiji la Dodoma walichangia shilingi milioni 4.2 hivyo jumla ya kiasi kilichotumika kuwa shilingi milioni 88.2
Bwana Mgingi amesema kuwa mbali na ujenzi wa bwalo hilo la wanafunzi shirika lake pia lilihusika katika ujenzi wa nyumba za walimu na kuwawekea umeme wa jua katika eneo la Losinoni Arusha, na katika mkoa wa Dodoma katika shule za Mlimwa A na B, Kiwanja cha Ndege na Chikoa katika halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo madarasa na samani zilitolewa katika shule hizo kwa vipindi tofauti.
Shirika la CDTF lilianzishwa mwaka 1962 na Mwanamke mwenye asili ya America Bibi Marion Lady Chesham na kwa muda wote huo limekuwa likishirikiana bega kwa bega na serikali za awamu zote katika kusaidia miradi ya maendeleo.
Shirika hili linaongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa sasa bwana Leon Msimbe ambaye alichukua uongozi huo kutoka kwa aliyekuwa spika mstaafu Mhe.Pius Msekwa. Miongoni mwa wadhamini wa kwanza wa shirika hili ni pamoja na Marehemu Rashid Kawawa, Spika wa kwanza Adam Sapi Mkwawa na Mzee Job Lusinde.