Home Siasa CCM DODOMA YAJIPANGA KUSHINDA KWA KISHINDO UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA,MBUNGE MAVUNDE...

CCM DODOMA YAJIPANGA KUSHINDA KWA KISHINDO UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA,MBUNGE MAVUNDE AMWAGA VIFAA VYA UCHAGUZI

0

Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Dodoma Mjini kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 kwa kuwafikia na kutatua kero,matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wake na pia kuwasimamia Viongozi wote wachaguliwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM na kutatua matatizo ya wananchi.

Hayo yamesemwa leo katika Ukumbi wa White House CCM Dodoma na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ndg Robert Mwinje wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya uenezi(Spika) na bendera kwa kata zote 41 vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Tunataka viongozi wote mliopo Serikalini na wawakikishi wa wananchi mnaotokana na CCM kuhakikisha mnatatua matatizo ya wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa ili tutengeneze uhalali kwa wananchi kuja kuwaomba ridhaa mwaka huu 2019 na mwakani 2020″Alisema Mwinje

Akitoa maelezo ya awali,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde amesema kwamba vifaa hivyo alivyotoa leo kwa kila kata na Uongozi wa Wilaya wa Jumuiya Speaker 45 zenye thamani ya Tsh 16,000,000 na bendera 1000 zenye thamani ya Tsh 3,500,000 ni maandalizi ya kampeni ya kisayansi ambayo wamepanga kuifanya katika Jimbo la Dodoma ili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi huu wa serikali za Mitaa.

“Kupendeza kwetu kwa mashati ya kijani na kuimba kwetu vizuri nyimbo za CCM hakuna maana kama hatutakua Chama cha kujibu kero za wananchi.Nimejipanga vizuri kuhakikisha naendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuhakikisha Jimbo la Dodoma Mjini linaendelea kutoa kura nyingi kwa CCM katika uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka 2020.Rais Magufuli na CCM imetufanyia mambo makubwa sana hapa Dodoma hususani Jimbo la Dodoma Mjini shukrani yetu tutailipa kwenye sanduku la kura”Alisema Mavunde

Wakati huo huo,Mbunge Mavunde ameahidi kutoka Tsh 20,500,000 kwa mgawanyo wa Tsh 500,000 kwa kata zote 41 katika kutunisha mfuko wa Uchaguzi wa Kata.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi wa Chama Wilaya na Viongozi wa Chama na Jumuiya zote kwa ngazi ya kata zote kwa Jimbo la Dodoma Mjini pamoja na Madiwani wa Kata na Viti Maalum.