Happy Lazaro, Dar es Salaam
Dar es Saalam .KAMPUNI ya Sab Gold Limited (SGL) imepanga kuanzisha mfumo wa pointi utakaowawezesha wachimbaji wadogo wa madini kupata huduma muhimu za uchimbaji ikiwemo kemikali, mitambo na vifaa kwa gharama nafuu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kuwaimarisha kiuchumi.
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Naasir Hussein, amesema mfumo huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwakani ambapo wachimbaji watakaowasilisha dhahabu kiwandani watakuwa wakikusanya pointi zitakazowawezesha kupata huduma kulingana na mahitaji yao.
Amesema kupitia utaratibu huo, mchimbaji anayehitaji kemikali au vifaa lakini hana uwezo wa kuvinunua ataunganishwa na kampuni zinazotoa huduma hizo, huku Sab Gold ikiratibu upatikanaji wake kwa gharama nafuu ili kupunguza changamoto na kuwakinga dhidi ya unyonyaji.
Hussein amesema wachimbaji wadogo ni injini ya sekta ya madini, akieleza kuwa takribani asilimia 40 ya shughuli za sekta hiyo zinategemea kundi hilo, hivyo wanahitaji kuwezeshwa kupitia ushirikiano wa serikali na sekta binafsi ili kuongeza mchango wao katika uchumi.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo pia inaona umuhimu wa dhahabu kutumika kama dhamana ya mikopo ili wachimbaji na wadau wengine wa sekta hiyo waweze kupata mitaji bila kutegemea hati za nyumba au mali nyingine pekee.
Amesema Sab Gold imeanza shughuli zake kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa takribani miezi mitano iliyopita, huku ikiwa tayari na orodha ya wachimbaji wapatao 120 hadi 130 katika eneo la Kahama na ikiendelea kutambua changamoto zao ili kuandaa huduma zinazokidhi mahitaji yao.
Hussein ameongeza kuwa mkakati wa kampuni hiyo ni kuanzia Kahama mkoani Shinyanga kabla ya kupanua huduma zake katika maeneo mengine ya uchimbaji ikiwemo Geita na Musoma, ili kuwafikia wachimbaji wengi zaidi, kuwaunganisha na fursa za kiuchumi na kuboresha maisha yao.
