Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
WAKALA wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umeendelea na kuhamasisha mama na baba lishe kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwemo mkaa mbadala, gesi na majiko ya umeme yanayotumia nishati kidogo, kwa lengo la kulinda afya zao na mazingira.
Akizungumza katika mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia yaliyofanyika Kigamboni, Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Bruno Tarimo, amesema taasisi hiyo imeamua kushiriki katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034.
Amesema mkakati huo uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan unalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, hivyo ni muhimu kwa makundi mbalimbali kushiriki katika kufanikisha azma hiyo.
Tarimo amesema mama na baba lishe ni kundi muhimu katika utekelezaji wa mkakati huo kutokana na shughuli zao za kila siku kuwahudumia wananchi wengi kupitia biashara za chakula, hivyo wanapaswa kupewa elimu na kuhamasishwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida.
Amesema Serikali imeweka msisitizo kuwa maeneo yanayohudumia zaidi ya watu 100 yanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.
Amebainisha kuwa matumizi ya mkaa mbadala yana faida mbalimbali, ikiwemo kupunguza ukataji wa miti, kulinda mazingira na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara kutokana na mkaa huo kudumu kwa muda mrefu wakati wa kupikia.
Aidha, amesema matumizi ya majiko ya umeme yaliyofanyiwa uhakiki na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni njia nyingine ya kuhamia kwenye nishati safi, kwani baadhi ya majiko hayo yameboreshwa kutumia umeme kidogo na kufanya kazi kulingana na uwepo wa chombo cha kupikia.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Tarimo amesema PBPA imeanza zoezi la kugawa tani 1,500 za mkaa mbadala kwa mama na baba lishe ili kuwawezesha kuanza kutumia nishati hiyo na kujionea manufaa yake katika shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kuwa wakala huo pia utatoa aproni kwa mama na baba lishe zitakazowasaidia kulinda mavazi yao wakati wa kupika na kuwa kumbusho la kuendelea kuzingatia matumizi ya nishati safi katika maeneo yao ya biashara na nyumbani.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mama na Baba nchini Lishe nchini Latifa Masasi ameishukuru PBPA kwa kuwakumbuka wafanyabiashara hao na kuwapatia elimu, akisema kundi hilo liko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema mama na baba lishe wanaendelea kuhitaji elimu ya mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya teknolojia na matumizi ya nishati salama, huku akiahidi kuwa chama hicho kitaendelea kuhamasisha wanachama wake kushiriki katika mafunzo na kutumia teknolojia hizo katika shughuli zao.
Nae Baba lishe Oswald Chanzi ameipongeza PBPA kwa kuwapa elimu hiyo huku akiwaomba kuhakikisha nishati hiyo mbadala waliowapatia inapatikana kirahisi na kwa gharama nafuu ili iwe na matumizi endelevu.

