Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kamati za Ushauri wa Kisheria Ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Msaada wa kisheria uliofanyika viwanja vya Sanawari Mataa mkoani Arusha Novemba 24, 2026.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari akimsikiliza mmoja wa wananchi wakati wa uzinduzi wa Kamati za Ushauri wa Kisheria Ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Msaada wa kisheria uliofanyika viwanja vya Sanawari Mataa mkoani Arusha Novemba 24, 2026
…………
Na Mwandishi Wetu, Arusha
WANANCHI 11,715 wamefikiwa kupitia kliniki za msaada wa kisheria zilizoanzishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mikoa tisa nchini, hatua inayolenga kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, kutatua migogoro kabla haijafikishwa mahakamani na kupunguza gharama za upatikanaji wa haki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kamati za Ushauri wa Kisheria Ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Msaada wa Kisheria mkoani Arusha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari, alisema idadi hiyo inaonesha umuhimu wa huduma hizo katika kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
Alisema kliniki hizo zimekuwa zikitoa huduma za bure kupitia mawakili wa serikali na wa kujitegemea, huku Mkoa wa Arusha ukiwa umeanza kupokea huduma hizo Novemba 24 hadi 29, 2026, katika Viwanja vya Sanawari jijini Arusha. Mikoa mingine iliyofikiwa ni Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Manyara, Simiyu, Dar es Salaam, Tanga, Katavi na Dodoma.
Johari alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Serikali inasikiliza wananchi, inatatua kero zao kwa wakati na kuweka mazingira yanayowawezesha kupata haki bila vikwazo.
Alifafanua kuwa kuanzishwa kwa kamati za ushauri wa kisheria katika ngazi za mikoa na wilaya kutasaidia kupokea na kuchambua malalamiko ya wananchi, kutoa elimu ya sheria na kutafuta suluhisho la migogoro kabla haijazalisha mashauri mahakamani, hatua itakayopunguza gharama kwa wananchi na Serikali.
Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa itakuwa na jukumu la kuratibu utekelezaji wa majukumu ya kamati za wilaya, kusikiliza malalamiko kuhusu upatikanaji na utoaji wa huduma za kisheria, kuwezesha wananchi kupata msaada wa kisheria na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Kamati hizo zitaundwa na wanasheria kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na taasisi nyingine za umma, wakiwemo wawakilishi wenye taaluma ya sheria kutoka vyombo vya usalama watakaoteuliwa na Mkuu wa Mkoa, pamoja na wajumbe wasio na taaluma ya sheria watakaoteuliwa kulingana na mahitaji ya eneo husika.
Katika ngazi ya wilaya, kamati zitakuwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na taasisi nyingine za umma, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya usalama na wajumbe wasio na taaluma ya sheria. Endapo mawakili wa serikali hawatakuwepo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Halmashauri husika atakuwa Mwenyekiti wa kamati.
Kamati hizo zinatakiwa kufanya vikao angalau mara moja kila robo mwaka, lakini jukumu la kusikiliza malalamiko na kutoa elimu ya sheria litaendelea wakati wote kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Pia zitaandaa kliniki za kisheria katika maeneo wanayoishi wananchi ili kuwafikia wale wanaoshindwa kufuata huduma katika ofisi za Serikali kutokana na umbali, gharama za usafiri au hofu ya kuingia katika ofisi hizo.
Akizungumzia umuhimu wa mfumo huo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo, alisema Serikali inalenga kupunguza migogoro ya ardhi na mashauri mengine yanayofikishwa mahakamani kupitia kamati hizo, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya mashauri yanayoshughulikiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yanahusu masuala ya ardhi.
Alisema kamati zitatoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha malalamiko yao, kupata ushauri na kutafuta ufumbuzi wa migogoro inayohusisha Serikali kabla haijafikia hatua ya mashauri ya mahakamani. Pia zitashauri viongozi na watendaji wa Serikali kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, alisema Serikali imeendelea kurahisisha upatikanaji wa haki kwa kutafsiri sheria zaidi ya 446 kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ili wananchi waweze kuelewa kwa urahisi haki na wajibu wao. Alisema hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ya lugha iliyokuwa ikiwafanya baadhi ya wananchi kushindwa kuelewa maudhui ya sheria na nyaraka mbalimbali za kisheria.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, George Mandepo, alisema mifumo 28 ya sheria inatarajiwa kufanyiwa mapitio na maboresho katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili iendane na mahitaji ya sasa na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku maeneo ya haki madai na haki jinai yakiwa miongoni mwa yatakayozingatiwa.
Akieleza mchango wa kampeni hiyo katika kujenga jamii yenye haki, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Bonaventura Mwambaja, alisema msaada wa kisheria unaendana na falsafa ya 4R ya Rais Samia inayosisitiza maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi upya. Alisema huduma hizo zinasaidia kutatua migogoro ya kifamilia, kupatanisha majirani na kuwasaidia wananchi waliokosa haki kwa muda mrefu, huku akitoa wito kwa wanasheria na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo.
Mwambaja alibainisha kuwa takwimu za Msajili na Chama cha Mawakili wa Serikali zinaonesha kuwa hadi Juni 2025, wananchi milioni 5.1 walikuwa wamefikiwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia nchini, wakiwemo wanawake milioni 2.7. Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Danford Mpelumbe, alisema tume hiyo inatarajia kufungua ofisi mkoani Arusha katika mwaka huu wa fedha ili kusogeza huduma za kulinda haki za binadamu na kusimamia utawala bora karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi – Serikali za Mitaa Mkoa wa Arusha, Nsajigwa Mwamnyange, aliwataka wajumbe wa kamati hizo kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, kujituma na kujitolea, akisisitiza kuwa uwepo wao katika ngazi za mkoa na wilaya utaimarisha juhudi zilizokuwa zikifanyika katika ngazi za halmashauri, kata, vijiji na vitongoji za kusikiliza na kutatua kero za wananchi. Wakati wa uzinduzi huo, Johari pia aliahidi kufuatilia malalamiko ya wananchi wawili, yakiwemo mgogoro wa soko la Kwa Sadala mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kuhakikisha wafanyabiashara wanapata nafasi ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

