Mwanasheria Mkuu wa serikali akisikiliza malalamiko ya mmoja wa wananchi Julius Ndewario baada ya uzinduzi huo jijini Arusha

…………
Na Happy Lazaro, Arusha
WANANCHI wawili, Julius Ndewario na Euralia Matai, mkazi wa Unga Ltd jijini Arusha, wamewasilisha malalamiko yao kuhusu migogoro ya ardhi inayowakabili, wakiiomba Serikali kuingilia kati ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazohusisha umiliki na uvamizi wa viwanja.
Malalamiko hayo yamewasilishwa wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Kudumu ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria bila Malipo mkoani Arusha, iliyofanyika katika viwanja vya Sanawari jijini Arusha, ambapo wananchi wamepata fursa ya kuwasilisha changamoto zao za kisheria kwa mamlaka husika.
Akieleza malalamiko yake, Julius Ndewario amesema amekuwa akimiliki na kulipia ada za Serikali kwa kiwanja chake bila kuwa na madai yoyote ya malipo kutoka Serikalini hadi msimu wa mwaka 2024/2025.
Amesema changamoto ilianza kujitokeza katika msimu wa mwaka 2025/2026 baada ya kubaini jina la mtu anayeitwa Joyce likionekana kwenye mfumo wa malipo, hali iliyomfanya kuhoji sababu za mabadiliko hayo na nafasi ya mtu huyo katika umiliki wa kiwanja husika.
Ndewario amesema anazo nyaraka za malipo na vielelezo vingine vinavyohusiana na kiwanja hicho, hivyo ameiomba Serikali kupitia kumbukumbu hizo ili kubaini chanzo cha mkanganyiko huo na kuhakikisha haki yake inalindwa.
Kwa upande wake, Euralia Matai, mkazi wa Unga Ltd jijini Arusha, ameeleza kukabiliwa na mgogoro unaohusisha viwanja vitatu ambavyo anadai amekuwa akivilipia, lakini vimevamiwa na watu wengine waliofanya shughuli za ujenzi.
Matai amesema kati ya viwanja hivyo, kimoja tayari kimejengwa na kukamilika huku watu wakiishi ndani ya nyumba zilizopo, huku viwanja vingine viwili navyo vikiwa vimeanza kuendelezwa kwa ujenzi kabla ya shughuli hizo kusimama baada ya jitihada zake za kufuatilia haki yake.
Amesema amefanya juhudi mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo, ikiwemo kufikisha malalamiko katika ofisi za Serikali na kupata msaada kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu, lakini licha ya hatua hizo suala hilo limeendelea kuwa na changamoto, ikiwemo kufikishwa mahakamani ambako anadai hakimu hakutambua madai yake.
Akijibu malalamiko hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari Hamza, amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepokea rasmi malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi hao na imeanza kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wengine wa Serikali ili kubaini kiini cha matatizo hayo na namna ya kuyatatua.
Hamza amesema ofisi yake itaendelea kuwa karibu na walalamikaji hao kwa mawasiliano na ufuatiliaji wa hatua zitakazochukuliwa, huku akiwataka kushirikiana na ofisi hiyo katika mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto walizowasilisha.
Ameeleza kuwa hatua hizo zitahusisha kupata taarifa na vielelezo muhimu kutoka kwa wahusika na maeneo husika ili kuwezesha uchunguzi na kubaini mazingira halisi ya migogoro hiyo, huku akiwapa pole kutokana na changamoto walizopitia.
Mwanasheria Mkuu wa serikali akisikiliza malalamiko ya mmoja wa wananchi Julius Ndewario baada ya uzinduzi huo jijini Arusha
