​Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kutoa huduma za Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha katika Viwanja vya Sanawari, Jijini Arusha tarehe 23 Novemba, 2026.

Kliniki hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kusogeza huduma mbalimbali za kisheria karibu zaidi na Wananchi.

Timu ya Mawakili wa Serikali na Wataalamu wa Sheria wako katika​ viwanja vya Sanawari, kutoa Ushauri wa Kisheria, elimu pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zikiwemo masuala ya ardhi, mirathi, ndoa, mikataba, na ajira kwa wananchi bila malipo.

Hatua hii ya kutoa huduma za kisheria bila malipo kwa wananchi, inadhihirisha dhamira ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za Kisheria kwa wananchi hususan wenye kipato cha chini, ambao wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kumudu gharama mbalimbali za huduma za sheria.

Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha itazinduliwa rasmi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, *Mhe. Hamza S. Johari* tarehe 24 Novemba, 2026 na itaendelea kutoa huduma kwa wananchi hadi tarehe 29 Novemba, 2026.

​Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Sanawari Jijini Arusha ili waweze kupata huduma mbalimbali za Kisheria, zinatolewa kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 23 hadi 29 Novemba 2026.