Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeiokolea Serikali Sh bilioni 8.86 kupitia ukaguzi wa gharama na mapato ya kampuni zinazojihusisha na utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, hatua inayolenga kuhakikisha Taifa linapata mapato stahiki kutokana na rasilimali hizo.

Fedha hizo ni sawa na Dola za Marekani milioni 3.3 zilizookolewa na kurejeshwa katika fungu la ugawanaji wa mapato baada ya ukaguzi uliofanyika katika vitalu vya Songo Songo, Namba 1 na 4 pamoja na Ruvuma, katika utekelezaji wa majukumu ya PURA kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza Novemba 23, 2026, jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema mafanikio hayo ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi unalinda maslahi ya Taifa.

Amesema PURA pia imekamilisha uandaaji wa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za hesabu za gharama na mapato ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia, unaojulikana kama PURA Cost Recovery Management System (CRMS), utakaorahisisha uwasilishaji, usimamizi na uhifadhi wa taarifa za kampuni zinazofanya shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini.

Katika kipindi hicho, PURA ilisimamia uzalishaji wa gesi asilia uliofikia futi za ujazo bilioni 65.4 katika vitalu vya Songo Songo na Mnazi Bay, ikilinganishwa na futi za ujazo bilioni 62.6 zilizozalishwa mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la bilioni 2.8.

Kwa mujibu wa taarifa ya PURA, ongezeko hilo lilichangiwa na kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya gesi asilia nchini, hususan viwandani na katika sekta ya usafiri kupitia matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).

Aidha, mamlaka hiyo ilisimamia uchimbaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, ambapo visima viwili vya MB-5 na MS-2 vilikamilika na kuanza uzalishaji, vikiwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 na milioni 50 kwa siku mtawalia.

Kisima cha tatu, Kasa-1X, kilichochimbwa kwa madhumuni ya utafutaji wa gesi asilia, kilibaini uwepo wa rasilimali hiyo inayokadiriwa kufikia futi za ujazo bilioni 223, hatua inayoongeza taarifa za uwepo wa gesi asilia katika eneo hilo.

Katika kuimarisha shughuli za utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia, PURA iliendelea kusimamia maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha Chikumbi-1, ukarabati wa kisima cha Ntorya-1 na majaribio ya uzalishaji katika kisima cha Ntorya-2, vyote vikiwa katika Kitalu cha Ruvuma.

Vilevile, PURA ilisimamia tafsiri mpya ya data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Tanga, ambapo matokeo yalibaini maeneo matatu yenye viashiria vya uwepo wa mafuta. Maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha utafutaji yanaendelea na yanatarajiwa kukamilika kwa uchimbaji mwaka 2027.

Katika maeneo ya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara, mamlaka hiyo ilisimamia ukusanyaji wa data za mitetemo kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi asilia. Hadi Juni 30, 2026, eneo la Eyasi-Wembere lilikuwa limekusanya kilomita 772 kati ya 779 zilizopangwa, sawa na asilimia 99, huku Lindi-Mtwara likiwa limekusanya data za mitetemo katika eneo la kilomita za mraba 257.96 kati ya 736.3, sawa na asilimia 35.

Kwa upande wa ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo, Mhandisi Sangweni amesema thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani katika miradi ya mkondo wa juu wa petroli mwaka 2026 ilizidi Dola za Marekani milioni 30, ikilinganishwa na milioni 14 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara mbili.

Amesema PURA pia ilisimamia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa majiko ya kisasa yanayotumia gesi ya LPG katika shule nne zilizopo Kata ya Msimbati, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, pamoja na ufadhili wa vijana kupata mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Lindi.

Ameongeza kuwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, PURA ilifanya mapitio ya Kanuni za Utafiti wa Awali na Utoaji wa Zabuni pamoja na Kanuni za Upangaji wa Bei ya Gesi Asilia, zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali Agosti 2025. Pia iliandaa kanuni zinazohusu uondoaji wa miundombinu ya petroli baada ya kumalizika kwa shughuli zake na uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.

Amesema PURA itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia, huku ikishirikiana na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha rasilimali hizo zinachangia ipasavyo katika kuongeza mapato ya Taifa, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi.