Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Novemba 21, 2026
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanywa kwa makusudi, huku akiwataka wakulima na wafugaji kuacha visasi, chuki na uhasama unaoweza kuhatarisha umoja wa Watanzania kutokana na migogoro ya ardhi.
Akizungumza katika Kata ya Bwilingu, wilayani Chalinze, mkoani Pwani, Novemba 21, 2026, baada ya mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete kuibua hoja ya kero ya wakulima na wafugaji na mipaka Mwigulu amesema kundi hilo linapaswa kuheshimiana na kuzingatia matumizi bora ya ardhi, akieleza kuwa ardhi ni rasilimali isiyoongezeka licha ya kuhitajika ndani ya jamii.
Mwigulu alieleza, migogoro hiyo haipaswi kugeuka chanzo cha kuvunjika kwa Utanzania wetu, akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutambua haki na wajibu wa mwenzake.
Ameongeza kuwa mfugaji anayeingiza mifugo katika mashamba ya wakulima au mkulima kupiga mifugo anafanya uchokozi na uvunjifu wa amani kwa makusudi, hivyo yeyote anayekiuka sheria achukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ametaja mgogoro wa mipaka kati ya Chamakweza na Pingo kuwa miongoni mwa kero za muda mrefu zinazohusisha jamii za wakulima na wafugaji.
Anasema viongozi mbalimbali wa mkoa na wizara wamekuwa wakiisimamia changamoto hiyo na kwamba sasa ni muhimu ipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Naibu waziri wa ardhi Kaspar Kaspar Mmuya ameeleza mipaka isiwe chanzo cha migogoro ama ugomvi.
Kaspar ameeleza vijiji 16 chalinze vipo katika bajeti ya kutengewa mpango wa matumizi bora ya ardhi huku akiwaasa wenyeviti wa vijiji kutoa ushirikiano wa utambuzi wa maeneo wakati wa mthamini wa ardhi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema Chalinze ni eneo la kimkakati katika biashara, viwanda na shughuli za madini ya kokoto, huku akieleza kuwa mkoa umeweka utaratibu wa kufanya kliniki za ardhi katika wilaya kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amebainisha kuwa Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zinazokabiliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji.

