Maafisa Viungo wa Taasisi za Muungano wametakiwa kuhudumia wananchi kwa karibu zaidi kupitia hatua itakayoimarisha Muungano wetu hivyo kupunguza malalamiko na changamoto zinazowakabili wananchi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi wakati wa ufunguzi wa kikao na maafisa viungo wa taasisi za Muungano kilichofanyika jijini Dodoma leo Novemba 19, 2026.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Dkt. Maduhu, Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Juma Mohamed Salum alisema wananchi wana matarajio makubwa kutoka kwa Serikali zote mbili ili waweze kunufaika na matunda ya Muungano.
Alisema kuwa kikao hicho kina lengo la kuwa na uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mambo ya Muungano na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Muungano ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa wakati.
“Kama mnavyofahamu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 nyongeza ya kwanza imeorodhesha maeneo 22 ya Muungano ambayo yanasimiwa na Taasisi za Muungano, hivyo Taasisi za Muungano ziana umuhimu mkubwa katika kuimarisha na kuendeleza Muungano kwa kuhakikisha ziantekeleza majukumu yake kwa weledi na kuhakikisha huduma zinatolewa pande zote mbili za Muungano, alisisitiza.
Aidha, Dkt. Juma alieleza kuwa kikao hicho kimefanyika katika wakati muhimu ambapo Serikali inaendelea kusisitiza uwajibikaji, ufanisi na matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya kila Taasisi.
Alisema Taasisi za Muungano zina wajibu mkubwa wa kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria zilizopo, hivyo alisisitiza ni jukumu la afisa kiungo wa taasisi kuhakikisha kuwa majukumu yanatekelezwa ili kuimarisha na kudumisha Muungano kwa kuzingatia misingi ya Muungano na maslahi mapana ya Taifa.
Halikadhalika, Dkt. Juma alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Maafisa Viungo wa Taasisi zote za Muungano kwani ni nguzo muhimu katika kuhakikisha masuala ya Muungano yanashughulikiwa kwa wakati, weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Hivyo, alisisitiza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa mwelekeo, uratibu na usimamizi unaohitajika ili Taasisi za Muungano ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

