Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa kampuni ya Kilimo Fresh Foods Africa , Baraka Chijenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo

……..

Na Happy Lazaro, Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa kampuni ya Kilimo Fresh Foods Africa , Baraka Chijenga amesema kampuni hiyo inapanga kupanua shughuli zake za biashara kwa kufungua huduma jijini Arusha na Zanzibar mwaka 2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza wigo wa soko la mazao ya kilimo nchini.

Akizungumza katika maonesho ya Kimataifa ya HortiLogistica 2026 yanayoendelea jijini Arusha, amesema kampuni hiyo ya Kitanzania inayotumia teknolojia kuunganisha wakulima na masoko kwa kununua mazao yao, kuyaongeza thamani kupitia usafishaji na ufungashaji kabla ya kuyasambaza kwa wateja.

Amesema kampuni hiyo yenye makao makuu Dar es Salaam inasambaza mazao kwa wateja zaidi ya 70 wakiwemo hoteli, migahawa, shule na supermarket, huku pia ikihudumia zaidi ya magenge 5,500 yanayouza mbogamboga na bidhaa za vyakula.

Ameongeza kuwa, kushiriki maonesho hayo kumekuwa na manufaa makubwa kwa kampuni hiyo kutokana na fursa ya kukutana na wakulima mbalimbali wa mazao ya bustani kutoka Arusha, ambao wameweza kubadilishana nao mawasiliano kwa ajili ya ushirikiano wa kibiashara wakati kampuni hiyo ikijiandaa kupanua huduma zake.

Amefafanua kuwa ,kupitia maonesho hayo wamefanikiwa kupata washirika katika maeneo ya usafirishaji, huduma za ugavi na uhifadhi wa mazao, hususani watoa huduma za cold storage, jambo litakalosaidia kuboresha uhifadhi na usambazaji wa mazao kwa ubora unaohitajika sokoni.

“maonesho hayo pia yamewasaidia kuelewa mahitaji ya soko la Arusha, aina ya mazao yanayopatikana na fursa zilizopo, hatua itakayowawezesha kupanga bidhaa watakazozipata katika eneo hilo na zile watakazozisambaza kutoka maeneo mengine.”amesema Chijenga .

Amesema upanuzi huo utakuwa fursa kwa wakulima na vijana wanaojihusisha na kilimo kushirikiana na kampuni hiyo, ambapo wakulima wataweza kuuza mazao yao moja kwa moja kwa kampuni huku watu wanaojihusisha na masoko wakipata nafasi ya kushirikiana katika kutangaza na kusambaza bidhaa zake.

Aidha, ameitaka Serikali kuongeza idadi ya maonesho ya biashara na kilimo katika maeneo mbalimbali nchini na kuyaimarisha zaidi ili yaweze kuwavutia wanunuzi, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania.

Amesema ni muhimu maonesho hayo kutangazwa kimataifa ili kuvutia washirika wa biashara katika sekta za usafirishaji, ufungashaji, uhifadhi na uwekezaji wa mitaji, jambo litakalosaidia biashara za ndani kukua na wakulima kupata masoko mapana zaidi.

 Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa kampuni ya Kilimo Fresh Foods Africa , Baraka Chijenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo