Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepata mafanikio mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, yakiwamo kuongezeka kwa wanyama adimu, kuimarika kwa ulinzi wa hifadhi, uwekezaji wa utalii na kuboreshwa kwa miundombinu.

Mafanikio hayo yamepatikana licha ya changamoto za ujangili, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Leo Novemba 10,2026 Jijini Dar es salaam katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massina Mwishawa, amesema shirika limefanikiwa kutekeleza doria 301,314 kati ya 314,940 zilizopangwa, zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 30,559 waliohusishwa na matukio 25,006 ya ujangili.

Amesema katika operesheni hizo, mifugo 65,860 iliyokuwa imeingia hifadhini kinyume cha sheria ilikamatwa, silaha 105 zilikamatwa na mitego ya nyaya 10,971 iliondolewa.

Mwishawa amesema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya wanyama adimu, ambapo faru wameongezeka kutoka 128 mwaka 2021 hadi wanaokadiriwa kufikia 170 mwaka 2026, huku sokwe waliozoeshwa wakiongezeka kutoka 196 hadi 288.

Ameongeza kuwa mbwa mwitu 25 wameachiwa katika maeneo yao ya asili, baada ya kuongezeka kutoka 12 waliokuwepo katika eneo la uzalishaji la Hifadhi ya Taifa Mkomazi.

Katika kuimarisha ulinzi, amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa ndege nyuki 40 kwa ajili ya doria za anga, pamoja na kujenga vituo vitatu vya mawasiliano na minara 10 ya redio. Teknolojia hiyo imesaidia kufuatilia makundi ya tembo na kuzuia matukio 9,787 yaliyoweza kuathiri wananchi.

Kwa upande wa utalii, amesema TANAPA imeongeza bidhaa za utalii kwa kuanzisha shughuli za utalii wa puto, faru, farasi, uvuvi wa kitalii, kuangalia nyota na safari za ndege za kutazama mandhari.

Aidha, amesema shirika limekamilisha ujenzi wa malango sita ya kuingilia wageni katika hifadhi mbalimbali na kuzindua uwanja wa gofu eneo la Fort Ikoma, Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Amesema uwekezaji wa malazi umeongezeka, ambapo idadi ya vitanda katika loji na kambi imepanda kutoka 5,755 mwaka 2021 hadi 12,094 mwaka 2026, huku maeneo mapya 160 ya uwekezaji yakitangazwa, yakiwamo loji 30 na kambi 130.

Katika kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi, TANAPA imetekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa zahanati tatu, nyumba mbili za waganga, vyumba viwili vya madarasa, bweni la wasichana na nyumba ya mwalimu, pamoja na kuweka mizinga 2,590 ya nyuki.

Pia, shirika hilo limewapatia mafunzo askari wa vijiji 410 kutoka vijiji 40, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa wananchi katika uhifadhi.

Hata hivyo, Mwishawa amesema TANAPA bado inakabiliwa na changamoto za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, uingizaji wa mifugo hifadhini, mimea vamizi, upungufu wa maji wakati wa kiangazi, ujangili na uharibifu wa miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, shirika litaongeza doria, kushirikiana na vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi, kuondoa mimea vamizi kwa kutumia mbinu za kisayansi na kujenga mabwawa pamoja na visima virefu kwa ajili ya maji ya wanyamapori.

Ameeleza kuwa mikakati mingine ni kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia, kuboresha barabara na viwanja vya ndege, kuongeza vituo vya askari na kujenga vizimba vya kuzuia mamba na viboko, huku likiwakaribisha wawekezaji kuwekeza zaidi katika hifadhi za Kusini, Mashariki na Magharibi ili kukuza utalii na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.