Na Mwamvua Mwinyi , Kibaha
Nov 10,2026

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha ,Fadhil Nkurlu amewataka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) kupeleka huduma kwa wananchi wa Mtaa wa Saeni na Karabaka Kata ya Misugusugu kufikia mwezi Disemba.

Ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Misugusugu, ambapo Mhe Nkurlu aliweza kupokea kero na changamoto mbalimbali zinazopatikana ndani ya maeneo hayo.

Nkurlu amesema TANESCO na DAWASA wahahakikishe kufikia Disemba maeneo ambayo yana changamoto ya maji na umeme inamalizika kwani kwa sasa Kibaha ni Manispaa hawawezi kuona wananchi wanaendelea kukaa gizani.

Kwa upande wa TANESCO na DAWASA, wamemuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa ifikapo Disemba wananchi wataanza kupata huduma hizo ambapo tayari miundo mbinu ilishawekwa ilibakia ni hatua chache za umaliziaji na hela imeshapatikana.

Aidha, katika mkutano huo wananchi wameweza kuwasilisha changamoto ya uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wamiliki wa Viwanda ambapo Mkuu wa Wilaya Nkurlu ameeleza kuwa Ofisi yake iko katika hatua za kuwaita wamiliki wote wa viwanda na kufanya nao kikao ili kuona ni kwa namna gani wanamaliza tatizo hilo hususani utiririshaji wa maji katika makazi ya wananchi.

Katika masuala mengine mbalimbali akipokea maswali kutoka kwa wananchi kuhusu kituo cha Polisi na Ujenzi wa Soko , Nkurlu amesema wananchi wa Kata ya Misugusugu watafute eneo ambalo wataona linafaa kwa ujenzi wa kituo cha Polisi pamoja na soko.

Akijibu swali la mwananchi kuhusu kituo cha Polisi, Mhe Nkurlu amesema wananchi watakapoamua kuanza ujenzi wa kituo hicho yeye binafsi atawachangia kwani maendeleo yanaletwa na wananchi wenyewe.

Kwa upande wa Diwani wa Viti Maalum Mhe Sarah Uledi amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika katika Kata yao na kusikiliza kero na changamoto za wananchi anaamini ujio wake umekuwa na faraja kubwa sana na umeweza kutoa majibu yaliyokuwa na sintofahamu kwa mida mrefu hususani maji na umeme.

Mkuu wa Wilaya amefanya mkutano huo wa hadhara na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magongwa, Mtendaji wa Kata, watendaji wa mitaa, wenyeviti wa serikali za mitaa na watalaamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha