Meneja mkuu wa kampuni ya Avo Africa, Nagib Karmali akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Wageni mbalimbali wakipata maelezo kwenye banda hilo juu ya umuhimu wa kuwekeza kwenye zao la parachichi .
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Meneja mkuu wa kampuni ya Avo Africa, Nagib Karmali, amewahimiza wakulima nchini kuwekeza katika kilimo cha parachichi akisema zao hilo lina fursa kubwa ya kibiashara kutokana na kuongezeka kwa mahitaji katika masoko ya kimataifa.
Karmali amesema kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni zinazofanya biashara ya parachichi nchini na kwamba kwa mwaka huu imefanikiwa kusafirisha karibu asilimia 50 ya parachichi zote zilizosafirishwa kutoka Tanzania kwenda katika masoko ya nje.
Amesema licha ya mahitaji makubwa ya zao hilo katika soko la kimataifa, uzalishaji wa ndani bado hautoshelezi mahitaji yaliyopo, hali inayofungua fursa zaidi kwa wakulima wanaotaka kuwekeza katika kilimo hicho.
“kampuni hiyo ina mahitaji ya takribani makontena 600 ya parachichi kwa mwaka, lakini kwa sasa inafanikiwa kupata na kukidhi mahitaji ya zaidi ya makontena 300 pekee, kutokana na upungufu wa parachichi zinazozalishwa nchini.”amesema Karmali.
Karmali amesema hali hiyo inaonesha kuwa bado kuna nafasi kubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa parachichi ili kunufaika na soko hilo, badala ya kusita kuwekeza kutokana na hofu ya kukosa wanunuzi wa uhakika.
“Avo Africa imejikita katika masoko makuu ya India, Mashariki ya Kati na Ulaya, ambako kuna mahitaji ya zao hilo, huku kampuni hiyo ikiendelea kuongeza juhudi za kupata mazao kutoka kwa wakulima wa ndani.”amesema Karmali.
Karmali ameongeza kuwa kampuni hiyo inakusanya parachichi kutoka maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Arusha, Moshi, Ngara na Kabanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wakulima wengi na kuongeza upatikanaji wa mazao kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.
Aidha amewataka wakulima, wasikate tamaa wala kuacha kulima parachichi huku akisisitiza kuwa uwepo wa soko na mahitaji makubwa ya zao hilo ni fursa muhimu ya kiuchumi inayopaswa kutumiwa na Watanzania.

