Mkurugenzi wa Shambarai Green Haven Ltd , Neema Kinabo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Mkurugenzi wa Shambarai Green Haven Ltd , Neema Kinabo, amesema soko la kimataifa lina uhitaji mkubwa wa mazao ya bustani (horticulture), hali inayotoa fursa kwa wakulima nchini kuongeza uzalishaji na kujikita katika kilimo cha mazao yanayokidhi mahitaji ya wanunuzi wa nje ya nchi.
Kinabo amesema licha ya kuongezeka kwa mahitaji ya mazao hayo katika masoko ya kimataifa, uzalishaji wa sasa bado hautoshelezi mahitaji yaliyopo, hivyo kuwapo kwa nafasi kubwa kwa wakulima na kampuni nyingine kuwekeza katika sekta hiyo na kunufaika na fursa za biashara ya mazao ya kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha,amesema Shambarai Green Haven Ltd lililopo Arusha linajihusisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, likilenga kutumia fursa zilizopo katika masoko ya kimataifa.
Neema amesema miongoni mwa mazao wanayozalisha kwa ajili ya masoko ya nje ni pilipili za aina mbalimbali, bitter gourd, matangokoi na ravaya, ambayo husafirishwa kwenda Israel na nchi nyingine, kutokana na mahitaji yaliyopo katika masoko hayo.
Ameeleza kuwa wamejikita katika kuzalisha aina mbalimbali za mazao ili kukidhi mahitaji ya wateja katika masoko ya kimataifa, huku wakiendelea kutambua fursa za mazao mengine yanayoweza kuuzwa nje ya nchi.
“Mbali na uzalishaji unaolenga soko la kimataifa, Kinabo amesema shamba hilo pia linazalisha ndizi na maparachichi kwa ajili ya soko la ndani, pamoja na nyanya, bitumbi, butternut na aina mbalimbali za saladi zinazotumika katika masoko ya mazao ya chakula.”amesema Neema.
Amesema mahitaji ya bidhaa hizo yanaendelea kuwa makubwa, huku kampuni yao ikiwa miongoni mwa kampuni chache zinazojihusisha na usafirishaji wa baadhi ya mazao hayo kwenda nje ya nchi, jambo linaloonesha uwepo wa fursa ambazo bado hazijatumika kikamilifu.
Aidha amesisitiza kuwa changamoto iliyopo si ukosefu wa soko, bali ni kiwango cha uzalishaji ambacho bado hakijaweza kukidhi mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa, hivyo kuwataka wakulima kuchangamkia fursa hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani yanayohitajika katika masoko ya nje na ndani ya nchi.
