Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo, amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), imefanikiwa kudhibiti mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya baada ya operesheni zilizofanyika Tanzania na Kenya na kukamata jumla ya paketi 753 za dawa hizo pamoja na watuhumiwa saba.
Amesema operesheni hizo zilianza Novemba 6, 2026, katika eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, ambapo watuhumiwa wanne walikamatwa wakiwa na paketi 299 za dawa za kulevya, zikiwemo paketi 24 za heroin na paketi 275 za methamphetamine.
Lyimo amesema dawa hizo zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo pia yanashikiliwa na mamlaka kutokana na kuhusishwa na uhalifu huo.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa ni Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda na dereva mkazi wa Piji, Uganda; Issa Said Nassoro (34), mfanyabiashara; Ibrahim Said Chembela (30), dereva; na Mohamed Ally Shemtuu (45), dereva, ambao watatu wa mwisho ni wakazi wa Tabata, Dar es Salaam.
Lyimo amesema baada ya kuhojiwa, watuhumiwa hao walieleza kuwa dawa hizo walizichukua Mombasa, Kenya, na kuzisafirisha kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, hatua iliyoiwezesha DCEA kuwasiliana na mamlaka za Kenya kwa ajili ya kubaini chanzo cha dawa hizo na kuwakamata wahusika wengine wa mtandao huo.
Kutokana na ushirikiano huo, Novemba 7, 2026, DCEA kwa kushirikiana na NANB walifanya operesheni eneo la Kwale, Mombasa, Kenya, na kufanikiwa kukamata paketi 454 za methamphetamine pamoja na watuhumiwa wengine watatu.
Watuhumiwa hao ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu kama Mbwiga, raia wa Tanzania na mfanyabiashara mkazi wa Mombasa; Seif Said Hamad (54), maarufu kama Babu Seif, raia wa Tanzania na mvuvi mkazi wa Kinondo, Mombasa; na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda na mfanyabiashara mkazi wa Shirazi, Mombasa.
Amesema taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Aidha, amesema baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa ni vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ambao umekuwa ukifanya shughuli zake katika nchi mbalimbali zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.
Lyimo ameeleza kuwa Saleh Khamis Baseleman, maarufu Mbwiga, anadaiwa kununua dawa za kulevya moja kwa moja nchini Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi katika fukwe za Mombasa, Kenya, kabla ya kuzisambaza katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Amebainisha kuwa Mbwiga pia anahusishwa na ukamataji wa tani 3.5 za dawa za kulevya uliofanywa na DCEA Desemba 2023 katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, na mkoani Iringa.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara na matumizi ya dawa hizo. 

