Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amezindua kiwanda cha nishati safi na salama cha Rafiki Briquettes kilichopo Wilaya ya Dodoma, Kata ya Chigongwe, mkoani Dodoma, huku akipongeza mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza Novemba 7, 2026, Waziri Mavunde amesema STAMICO ambayo awali ilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyokuwa yakitajwa kufutwa kutokana na kutokuwa na tija, sasa imebadilika na kuongeza mapato kutoka Sh bilioni moja hadi zaidi ya Sh bilioni 89. Amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi wa Dkt. Venance Mwase na timu yake, huku akiwataka kuongeza juhudi ili STAMICO iwe na nguvu ya kushindana na kampuni kubwa za madini kama Geita Gold Mine, Barrick, Shanta na Twiga.
Aidha, Mavunde amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imeiwezesha STAMICO kwa kuipatia leseni mbalimbali za madini, ikiwemo dhahabu katika Pori la Kigosi, madini ya dimu Morogoro na nickel maeneo ya Ntakanga na Chimbwera. Amesema STAMICO inatarajiwa kuanza miradi hiyo kwa kasi na kuongeza mapato ya shirika, huku akieleza kuwa matarajio yake ni kuliona shirika hilo likiwa na nguvu sawa na kampuni kubwa za madini ndani ya miaka mitatu ijayo.
Katika hatua nyingine, Mavunde ameitaka STAMICO kuendelea kuwekeza katika nishati safi na salama, ikiwemo uzalishaji wa briquettes zinazoweza kupunguza matumizi ya mkaa na ukataji miti. Pia ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha shughuli zake zinawanufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo wanayofanyia kazi, akielekeza STAMICO kushiriki katika ujenzi wa shule na kuboresha huduma za jamii, ikiwemo kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari katika eneo la Chigongwe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Madini kupitia STAMICO kwa ubunifu wa kuzalisha mkaa rafiki wa mazingira, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Aidha,kwa niaba ya kamati ametoa maelekezo kwa STAMICO kuendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati kupitia REA, akitaka majiko banifu yanayotolewa kwa ruzuku yaendane na matumizi ya mkaa huo wa briquettes, huku akisema Kamati hiyo itawasiliana na kamati zinazoshughulikia Wizara ya Elimu na TAMISEMI ili kuongeza idadi ya taasisi zinazotumia nishati safi ya kupikia.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Simon Sirro, amesema shirika hilo limepiga hatua kubwa katika kipindi kifupi, ikiwemo kusaini mikataba minne ya kuendeleza leseni za madini mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/2026. Amesema kiwanda kilichozinduliwa ni cha nne cha uzalishaji wa nishati safi ya kupikia baada ya vile vya Tuwila, Kilosa na Tabora, huku akipongeza Menejimenti ya STAMICO kwa kazi kubwa ya kuimarisha shirika na kuhakikisha miradi yake inawanufaisha Watanzania.
Balozi Sirro amesema changamoto iliyopo sasa ni suala la masoko na kuitangaza bidhaa hiyo, hivyo amemuomba Waziri wa Madini kusaidia STAMICO kupata masoko ya uhakika, hasa katika shule za vijijini ambazo bado zinatumia kuni. Aidha, amewataka Watanzania kutumia nishati hiyo safi na salama ya kupikia kwa gharama nafuu na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ili kutunza mazingira, hatua ambayo pia itaunga mkono azma ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Awali, Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, amesema kiwanda hicho kipya cha kuzalisha nishati safi ya kupikia aina ya Rafiki Briquettes kina uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa na kimegharimu Sh bilioni 3.7, huku vifaa vyote vilivyozinduliwa katika tukio hilo vikiwa na thamani ya Sh bilioni 6.09.
Dkt. Mwasse amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za STAMICO kuongeza thamani ya madini ya makaa ya mawe na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku akieleza kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takribani watu 100, wengi wao wakiwa vijana wa eneo la Chigongwe, pamoja na kutoa fursa za biashara katika usafirishaji, usambazaji na upatikanaji wa malighafi.
Aidha, amesema STAMICO inaendelea kupanua uzalishaji wa Rafiki Briquettes nchini, ikiwa tayari ina mawakala 92, huku akibainisha kuwa kilo moja ya bidhaa hiyo inauzwa kiwandani kwa Sh 800 na kwa mtumiaji wa mwisho Sh 1,000, ikiwa na uwezo wa kuwaka kwa zaidi ya saa tatu. Amesema bidhaa hiyo inalenga kuchangia kufikia lengo la Taifa la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

