Mkuu wa mkoa wa Arusha,CPA Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo kuhusu jukwaa hilo.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Bustani Tanzania (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .MAKAMU wa Rais Mhe. Deogratius John Ndejembi anatarajiwa kuwa mgenirasmi katika Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, litakalofanyika Novemba 8 hadi 10 katika viwanja vya TGT jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika viwanja vya TGT jijiji Arusha ,Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amesema kuwa ,jukwaa hilo linatarajiwa kushirikisha waoneshaji zaidi ya 150 kutoka Afrika, Ulaya na Asia pamoja na wageni zaidi ya 3,000 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani.
CPA Makalla amewakaribisha wadau wa sekta ya kilimo, wawekezaji, wafanyabiashara na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi mkoani Arusha, kushiriki Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026.
“jukwaa hilo litafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, atakayekuwa mgeni rasmi na ujio wake unaonesha umuhimu wa sekta ya horticulture katika kukuza uchumi, ajira na biashara ya kimataifa.”amesema CPA Makalla.
CPA Makalla amesema HortiLogistica Africa 2026 ni fursa kubwa ya kukuza uchumi wa Arusha kupitia biashara, uwekezaji na utalii.
Amesema mbali na kukuza biashara ya matunda, mboga, viungo na maua, jukwaa hilo litachochea shughuli za uwekezaji, hoteli, usafirishaji na utalii, huku likiimarisha nafasi ya Arusha kama kitovu cha biashara na matukio ya kimataifa, akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujitangaza, kujenga mahusiano ya kibiashara na kunufaika na washiriki wa jukwaa hilo la Kimataifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Bustani Tanzania (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi, amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya kimataifa, teknolojia za kisasa, wawekezaji na watoa huduma za usafirishaji ili kuongeza ushindani na thamani ya mazao ya Tanzania.


