NA DENIS MLOWE, IRINGA
SHULE ya Awali na Msingi ya Good Victory iliyopo Manispaa ya Iringa inayoshika nafasi ya kwanza kila mwaka kimkoa tangu kuazishwa kwake 2018 mefanya mahafali ya wanafunzi wake wa awali katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa shule hiyo, huku ikieleza mafanikio mbalimbali iliyoyapata katika taaluma, malezi na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mwanaidi Hamza, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kushirikiana na walimu katika malezi na ulinzi wa watoto ili kuhakikisha wanakua katika mazingira salama yenye misingi bora ya maadili.
Hamza amesema malezi ya watoto yanahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi na jamii kwa ujumla, akieleza kuwa changamoto zinazowakabili watoto katika jamii ya sasa zinahitaji juhudi za pamoja ili kuwalinda na kuwaandaa kuwa raia wenye uwajibikaji.
Ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kufuatilia mienendo na maendeleo ya watoto wao, kuwapa mwongozo unaofaa na kushirikiana na walimu pale wanapobaini changamoto zinazohitaji hatua za pamoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo, Emmanuel Nyingi, amesema Good Victory imejikita katika kutoa elimu bora inayozingatia mahitaji ya mtoto, huku ikilenga kumwandaa mwanafunzi kitaaluma na katika masuala ya malezi na makuzi.
Nyingi amesema mafanikio ya shule hiyo yanatokana na ushirikiano wa uongozi, walimu, wazazi na walezi, akiwashukuru wazazi kwa kuendelea kuiamini shule na kutimiza wajibu wao katika kulipia ada kwa wakati ili kurahisisha utoaji wa huduma za elimu.
Amesema shule inaendelea kuboresha huduma zake kwa kuwekeza katika teknolojia, ikiwemo kuanzisha darasa la kompyuta na kuimarisha mifumo ya usalama kwa kuweka kamera za CCTV katika mazingira ya shule.
Naye Meneja wa shule hiyo, Eunice Kimathi, amesema kulea watoto ni jukumu linalohitaji kujituma na uwajibikaji mkubwa, akiwashukuru walimu na wafanyakazi wote kwa mchango wao katika kuwalea na kuwaandaa wanafunzi kitaaluma.
Kimathi amesema wanafunzi wanaohitimu elimu ya awali wamejengewa msingi wa kusoma, kuandika na kuhesabu, huku shule ikiendelea kuandaa mazingira rafiki yatakayowawezesha wanafunzi kukua na kufikia malengo yao ya kielimu.
Akizungumzia mafanikio ya kitaaluma, Mwalimu Mkuu wa Good Victory, Sabato Thomas, amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa miaka mbalimbali, ikipata nafasi za juu katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.
Thomas amesema katika matokeo ya darasa la nne ya mwaka 2025, shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza wilayani na kimkoa na nafasi ya tatu kitaifa, huku mwaka 2026 wanafunzi 95 wakifanya mtihani wa upimaji wa kitaifa.
Amesema katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2024 na 2025, wanafunzi wa shule hiyo walifaulu kupata alama A katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, huku katika matokeo ya mwaka 2026 wanafunzi wote waliofanya mtihani huo wakipata alama A, na kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya kwanza wilayani na kimkoa katika kundi la shule zenye wanafunzi zaidi ya 40.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maandalizi ya kutosha kwa wanafunzi na walimu, ikiwemo tathmini za kila somo, pamoja na ushirikiano wa wazazi, wafanyakazi na mamlaka za elimu katika ngazi mbalimbali.
Aidha, amesema shule imeendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kuanzisha darasa la kompyuta, kuweka vifaa vya teknolojia na kufunga kamera za CCTV kwa lengo la kuimarisha usalama wa wanafunzi na mali za shule.
Mahafali hayo yamekuwa sehemu ya kutambua hatua iliyofikiwa na wanafunzi katika safari yao ya elimu, huku uongozi wa Good Victory ukiahidi kuendelea kuimarisha ubora wa elimu, malezi na mazingira ya kujifunzia ili kuwaandaa watoto kukabiliana na changamoto za maisha ya baadaye.
