Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetakiwa kutumia kikamilifu uhusiano mzuri wa Tanzania na mataifa mbalimbali duniani kuvutia uwekezaji, kuendeleza rasilimali za nchi zilizopo nje ya mipaka na kuongeza mapato ya Taifa kupitia miradi ya kiuchumi. Hatua hiyo inalenga kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha diplomasia inayochochea maendeleo ya kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, Novemba 6, 2026, alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la ghorofa 22 linalomilikiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya. Katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mmuya alisisitiza kuwa ardhi na majengo yanayomilikiwa na Serikali kupitia balozi za Tanzania nje ya nchi yanapaswa kuendelezwa na kutumika kiuchumi badala ya kubaki bila kuleta manufaa. Alieleza kuwa rasilimali hizo zinaweza kuwa vyanzo muhimu vya mapato kupitia uwekezaji na shughuli za biashara.

Aidha, alihimiza Wizara kuimarisha ushirikiano na wawekezaji pamoja na taasisi za kifedha ili kupata mitaji ya kuendeleza miradi hiyo katika balozi nyingi zaidi, huku akipongeza hatua ambazo tayari zimeanza kutekelezwa katika baadhi ya balozi za Tanzania.

Alibainisha kuwa uwekezaji katika rasilimali hizo hautaongeza tu mapato ya fedha za kigeni, bali pia utaimarisha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi husika, kufungua fursa mpya za biashara na kuiwezesha nchi kupata uzoefu wa kusimamia miradi ya kibiashara katika masoko ya kimataifa.

Mhe. Mmuya aliipongeza Wizara kwa juhudi za kutekeleza maono ya Rais Samia katika kukuza diplomasia ya kiuchumi. Vilevile, alimpongeza Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibese, kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya diplomasia hayapaswi kupimwa kwa kujenga uhusiano na urafiki pekee, bali pia kwa uwezo wa kugeuza uhusiano huo kuwa fursa za uwekezaji, biashara na mapato yanayochangia maendeleo ya Taifa.