*Ni katika kuboresha hali ya upatikanaji umeme kwenye maeneo yaliyoathirika 

*MD Twange awashukuru wateja na kuahidi kuhakikisha huduma inarejea katika hali ya kawaida

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikisha kwa haraka ujenzi wa njia nyingine ya muda ya kusafirisha umeme ya juu (overhead) ikiwa ni juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wateja wa maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti, waliokumbwa na changamoto iliyojitokeza kwenye njia ya kusafirisha umeme chini ya ardhi yenye msongo wa kilovoti 132 (132kV) katika eneo la Gongolamboto.

Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa TANESCO kubuni na kuanza kutekeleza njia hyo mbadala ya muda wa kusafirisha umeme kwa njia ya juu, unaovuka eneo la miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), ili kufidia sehemu ya njia ya chini ya ardhi iliyopata hitilafu na kuhakikisha wateja wanaendelea kupata huduma ya umeme wakati matengenezo yakiendelea.

Akizungumza leo, tarehe 7 Novemba 2026, wakati wa akikagua maendeleo ya kazi za matengenezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amepongeza jitihada za wataalamu wa Shirika kwa kujenga kwa haraka na kutekeleza suluhisho hilo la dharura ili kupunguza changamoto kwa wateja walioathirika.

Amesema TANESCO inaendelea kuchukua hatua za kiufundi kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa wateja wakati wote, huku kazi za kurekebisha miundombinu iliyoharibika zikiendelea.

“Tumefika hapa kukagua maendeleo ya kazi na kujionea hatua zinazochukuliwa na wataalamu wetu. Tumefarijika kuona kuwa wameweza kutengeneza njia nyingine mbadala ya juu inayovuka eneo la SGR ili kuhakikisha umeme unaendelea kusafirishwa na kuwafikia wateja wetu wakati matengenezo ya njia ya ardhini yakiendelea. Tunawahakikishia wateja wetu kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata huduma ya umeme,” amesema Bw. Twange.

Aidha, amesisitiza kuwa TANESCO inaendelea kuimarisha miundombinu yake na kutafuta suluhisho zinazopunguza athari kwa wateja pale changamoto za kiufundi zinapojitokeza, akibainisha kuwa kuridhika kwa wateja na upatikanaji wa huduma ya uhakika ni kipaumbele cha Shirika.

Kwa upande wake, wataalamu wa TANESCO wameendelea na hatua za kuunganisha na kukamilisha mfumo huo mbadala, kazi inayohitaji tahadhari na kufanyika kwa kuzingatia taratibu za usalama ili kuhakikisha njia hiyo inakuwa tayari kutumika kwa ufanisi.

Hitilafu hiyo ilianza kujitokeza Novemba 3, 2026, katika njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 inayounganisha Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto na vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni.Ambapo Changamoto hiyo iliathiri upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti kutokana na njia mbadala iliyokuwepo awali kuwa na uwezo mdogo wa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja.

TANESCO inaendelea na juhudi za kurekebisha miundombinu hiyo kwa lengo la kurejesha hali ya kawaida na kuimarisha uhakika wa huduma ya umeme kwa wateja wake.