Na Mwandishi Wetu , Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill M. Kiwia, amesema wanafunzi 14 kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamepata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kupitia Ngorongoro Scholarship Fund kwa mwaka wa masomo 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu kwa jamii hiyo na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika maendeleo na uhifadhi.

Akizungumza Novemba 7, 2026, katika hafla ya kuwapongeza na kuwatambua wanafunzi hao iliyofanyika katika Ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam, Dkt. Kiwia amesema jumla ya Sh milioni 70.6 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo mwaka huu, ambapo kwa mara ya kwanza wanafunzi 14 wamekidhi vigezo na kunufaika na ufadhili huo.

Amesema mpango huo ni matokeo ya ushirikiano kati ya HESLB na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambao ulirasimishwa kupitia hati ya makubaliano ya ushirikiano na kuhusisha maandalizi ya mwongozo wa ufadhili, utoaji wa elimu kwa jamii, upokeaji wa maombi na tathmini ya waombaji ili kuhakikisha fursa hiyo inawafikia wanafunzi wenye sifa zinazostahili.

Dkt. Kiwia amewapongeza wanafunzi hao na kuwataka kutumia fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili na kufikia malengo yao ya kitaaluma, huku akisisitiza kuwa baada ya kuhitimu wanatarajiwa kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata kuchangia maendeleo ya Ngorongoro, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa Taifa.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Abdul-Razaq Badru, amesema wanafunzi hao ni wananchi wa eneo la hifadhi walionufaika na mfuko huo kwa mwaka wa masomo 2026/2027, ambapo jumla ya Sh milioni 100 zimetengwa na wanafunzi 14 tayari wameripoti katika vyuo mbalimbali na kuanza masomo yao.

Dkt. Badru amesema ufadhili huo unalenga kuwawezesha wananchi wenye sifa lakini wasiokuwa na uwezo wa kugharimia elimu ya juu, kwa kuwapatia nafasi ya kusoma fani zinazohusiana na uhifadhi wa wanyamapori na misitu, malikale na utalii, ambazo zitawawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Amesema kutokana na sheria za uhifadhi, wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamekuwa wakitegemea zaidi ufugaji kama shughuli yao kuu ya kiuchumi, lakini hali ya maisha imeonesha kuwa shughuli hiyo pekee haiwezi kukidhi mahitaji yao, hivyo elimu ni njia mbadala ya kuwafungulia fursa nyingine za kiuchumi na ajira nje ya hifadhi.

Dkt. Badru amesema Ngorongoro Scholarship Fund ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu matatu ya NCAA ambayo ni uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii, huku akieleza kuwa mpango huo utaendelea kutekelezwa kila mwaka kwa kushirikiana na HESLB kwa kuzingatia mwongozo wa utoaji wa ufadhili wa masomo.

Ameongeza kuwa mpango huo ulianza kwa maandalizi yaliyohusisha NCAA na HESLB, ikiwemo kusaini hati ya makubaliano Januari 2026, kabla ya uzinduzi rasmi wa Ngorongoro Scholarship Fund uliofanyika Agosti 4 mwaka huu, akieleza kuwa hatua ya sasa ni utekelezaji wa makubaliano hayo kwa kuwapatia wanafunzi fursa ya elimu ya juu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa NCAA amewapongeza wanafunzi 14 na kuwatakia mafanikio katika masomo yao, huku akieleza kuwa elimu itakuwa msingi wa kuwawezesha vijana wa Ngorongoro kupata ujuzi, kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo zinazoweza kufanyika nje ya eneo la hifadhi.

Naye, Meneja Miradi wa HESLB, Bi. Gertrude Alphonce, amesema ufadhili huo ulianza kwa maandalizi ya pamoja kati ya HESLB na NCAA, ambapo taasisi hizo ziliandaa mwongozo, kubainisha sifa za wanufaika, kuweka vigezo vya ufadhili na kuandaa utaratibu wa kupokea na kushughulikia maombi ya wanafunzi.

Amesema HESLB na NCAA zilifanya ziara ya uhamasishaji na kutoa elimu kwa wananchi wa Ngorongoro kuhusu fursa hiyo, majukumu ya HESLB na masharti ya ufadhili, huku zikisikiliza maoni na changamoto za jamii ili kuhakikisha walengwa wanaelewa namna ya kuomba na kunufaika na mpango huo.

Bi. Alphonce amesema dirisha la maombi lilifunguliwa kuanzia Agosti 15 hadi Septemba 15, 2026 kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Mikopo na Ufadhili wa Wanafunzi (OLAMS), ambapo waombaji walitakiwa kuwa Watanzania, wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa angalau miaka minne, kudahiliwa katika taasisi zinazotambulika kwenye programu zilizoorodheshwa kwenye mwongozo na kuonesha uhitaji wa kifedha.

Amesema baada ya kupokea maombi, HESLB ilifanya uhakiki na tathmini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, huku akiwataka wanafunzi wanufaika kusoma mikataba yao ya ufadhili, kutia saini, kuzingatia programu walizodahiliwa na kutoa taarifa kwa HESLB endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote yanayohusu masomo yao.

Aidha, amesema malipo ya ufadhili yatafanyika kupitia mfumo wa Digital Disbursement Solution (DiDiS), ambapo ada za masomo zitalipwa moja kwa moja kwenye akaunti za taasisi husika na vipengele vingine vya ufadhili vitapelekwa kwenye akaunti za wanafunzi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya HESLB na NCAA utaendelea kuimarishwa ili kuongeza fursa za elimu kwa vijana wa Ngorongoro.