Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi na kuhamasisha ushiriki wao katika hatua mbalimbali za mtangamano wa kikanda.

Zoezi hilo lililofanyika Novemba 2, 2026, limefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Bw. Musa Ramadhani Sima, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, taasisi za dini, mashirika ya kiraia, vijana, wanawake na makundi maalum.

Kupitia zoezi hilo, washiriki wamepata fursa ya kufahamu misingi na malengo ya Fungamano la Kisiasa la EAC, pamoja na hatua zinazotarajiwa kufuatwa katika mchakato wa Katiba hiyo, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo yao.

Aidha, elimu hiyo inalenga kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa Fungamano la Kisiasa katika kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama wa EAC, huku ikitoa nafasi kwa makundi mbalimbali ya jamii kujiandaa kuchangia mawazo yatakayosaidia kufanikisha hatua zinazofuata.

Zoezi hilo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki za kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuelekea Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki.