Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel W. Shelukindo, amewahimiza watumishi wa Wizara hiyo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuimarisha afya, kuongeza ufanisi na kuwa na utayari wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Ametoa wito huo mara baada ya kushiriki mbio za Capital City Half Marathon 2026, zilizofanyika Novemba 1, 2026, katika viwanja vya Chimwaga jijini Dodoma, zikilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa michezo, afya na mshikamano.

Amesisitiza kuwa afya bora ni msingi muhimu wa utendaji kazi wenye tija, hivyo watumishi wanapaswa kuyafanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha yao badala ya kusubiri matukio maalumu ya michezo.

Aidha, amewataka watumishi wote wa Wizara kushiriki kikamilifu katika ratiba ya mazoezi ya pamoja inayofanyika kila Jumanne na Alhamisi, akieleza kuwa utaratibu huo ni fursa muhimu ya kuimarisha afya, kujenga mshikamano na kuongeza ari ya uwajibikaji mahali pa kazi.

Mbio za Capital City Half Marathon 2026 zimewakutanisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha mtindo bora wa maisha kupitia michezo na mazoezi ya viungo.