NA DENIS MLOWE, IRINGA

ABUU Changawa, mwanachama wa Simba Sports Club mwenye kadi namba 22924, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa uongozi wa klabu hiyo, akitaka maslahi ya wanachama na mustakabali wa timu kupewa kipaumbele katika maamuzi yanayohusu uwekezaji na usimamizi wa klabu.

Changawa anasema hayo wakati akizungumza na wanahabari mkoani Iringa juu ya mjadala unaoendelea kuhusu tofauti kati ya Bodi ya Wakurugenzi na Kamati ya Utendaji unahitaji kutazamwa kwa kina, kwa kuzingatia katiba ya Simba na nafasi ya wanachama katika kulinda mali na thamani ya klabu hiyo.

Akieleza msingi wa msimamo wake, Changawa anasema ana uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya soka, akiwahi kuwa kiongozi katika Kamati ya Maendeleo ya Michezo Manispaa ya Iringa, Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Iringa na mwakilishi wa vilabu katika ngazi ya manispaa pia amesema aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Lipuli kwa miaka minne, kipindi ambacho anasema alikamilisha muda wake wa uongozi bila kuondolewa kabla ya wakati, tofauti na ilivyokuwa kwa baadhi ya viongozi wengine wa klabu hiyo.

Changawa anasema alihudumu kwa miaka saba kama mjumbe wa bodi ya ligi chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), nafasi aliyopata kupitia uchaguzi wa vilabu na uteuzi wa uongozi wa bodi hiyo.

Anasema uzoefu huo umemwezesha kuelewa taratibu za uendeshaji wa klabu, mahusiano kati ya vyombo vya uongozi na umuhimu wa kuzingatia katiba katika kutatua migogoro.

THAMANI YA SIMBA YAZUA MASWALI

Akizungumzia suala la uwekezaji, Changawa amepinga kile anachokiona kuwa ni hatari ya kufanya maamuzi kuhusu umiliki wa Simba bila kuwepo kwa tathmini inayojitosheleza ya thamani halisi ya klabu hiyo.

Amedai kuwa thamani ya Simba inaweza kufikia Sh bilioni 250, akisisitiza kuwa kabla ya kujadili kiwango cha uwekezaji au hisa zitakazotolewa, ni muhimu kufanyika kwa tathmini ya kina ya mali, biashara na uwezo wa klabu kuzalisha mapato.

Changawa anasema Simba si timu ya mpira pekee, bali ni taasisi yenye wanachama na mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania, ambao kwa mtazamo wake ni sehemu muhimu ya mtaji wa klabu hiyo kutokana na hilo amehoji mantiki ya kujadili uwekezaji wa Sh bilioni 20 bila kuwa na taarifa za wazi zinazoonesha namna thamani hiyo ilivyopatikana na vigezo vilivyotumika kuamua kiasi cha uwekezaji kinachohitajika.

Anasema tathmini hiyo inapaswa kuzingatia mali za klabu, mapato yake, ukubwa wa wigo wa mashabiki na wanachama, pamoja na fursa za kibiashara zinazoweza kutumiwa kuongeza mapato.

WANACHAMA NI MTAAJI MUHIMU

Changawa amesisitiza kuwa wanachama na mashabiki ni miongoni mwa rasilimali muhimu zaidi za Simba, akieleza kuwa klabu inaweza kuongeza uwezo wake wa kifedha kwa kuimarisha ushiriki wa watu wanaoiunga mkono.
Kwa mfano, amesema iwapo Simba ingeweza kupata wanachama au mashabiki milioni moja wanaochangia Sh 10,000 kila mmoja, ingeweza kukusanya Sh bilioni 10.

Anaongeza kuwa iwapo idadi hiyo ingeongezeka hadi watu milioni mbili, kiwango cha fedha kingefikia Sh bilioni 20, jambo ambalo kwa mtazamo wake linaonesha umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kuimarisha mapato kupitia wanachama na mashabiki.

Hata hivyo, amesema mikakati hiyo inahitaji mipango madhubuti ya kuwashirikisha mashabiki, kuimarisha uaminifu na kuweka utaratibu wa wazi wa ukusanyaji na matumizi ya fedha.

Changawa anaeeleza kuwa uwekezaji unaofanywa na mtu binafsi haupaswi kutazamwa kama njia pekee ya kuendeleza klabu, bali unapaswa kwenda sambamba na juhudi za kuimarisha rasilimali zinazotokana na wanachama na shughuli za kibiashara.

Anasema uwekezaji unapaswa kujengwa juu ya tathmini ya uwezo wa mwekezaji na thamani ya klabu, huku maslahi ya wanachama yakilindwa kwa mujibu wa katiba na taratibu zilizowekwa.

APINGA MIGOGORO YA VYOMBO VYA UONGOZI

Kuhusu mgogoro unaodaiwa kuwepo kati ya Bodi ya Wakurugenzi na Kamati ya Utendaji, Changawa amesema tofauti hizo zinapaswa kutatuliwa kwa kuzingatia katiba ya Simba badala ya kuruhusu mvutano unaoweza kuathiri maendeleo ya timu.

Anadai kuwa katika mchakato wa uwekezaji, ni muhimu kuweka wazi majukumu ya kila chombo cha uongozi, namna kinavyopata mamlaka na mipaka ya maamuzi yake.

Anasema kuwa Kamati ya Utendaji inayochaguliwa na wanachama inapaswa kuzingatiwa katika masuala yanayohusu uendeshaji wa klabu, kwa mujibu wa katiba na mamlaka iliyokabidhiwa.

Anasema migogoro inayotokana na kutokubaliana kuhusu madaraka inaweza kuathiri umoja wa wanachama na kuibua mashaka kuhusu namna maamuzi muhimu yanavyofanywa.

Changawa ametoa wito wa kuwepo kwa uwazi katika mchakato wa uwekezaji, akitaka wanachama wapate maelezo ya kutosha kuhusu thamani ya klabu, masharti ya uwekezaji na athari zake kwa umiliki na uendeshaji wa Simba.

Amesisitiza kuwa maamuzi makubwa yanayohusu mustakabali wa klabu yanapaswa kufanywa kwa kuzingatia maslahi mapana ya taasisi hiyo na si maslahi ya kundi dogo la watu.

AHOJI NAFASI YA MO DEWJI

Akizungumzia nafasi ya Mohammed Dewji, maarufu kama Mo Dewji, Changawa amesema suala la uwekezaji linapaswa kutazamwa kwa kuzingatia mchango ambao mwekezaji anaweza kuutoa katika maendeleo ya klabu.

Anasema mtu anayetaka kuwekeza katika Simba anapaswa kuwasilisha mpango unaoonesha namna atakavyosaidia klabu kuongeza mapato, kuimarisha ushindani na kukuza thamani yake.

Kwa mtazamo wake, mwekezaji anapaswa kuja na mikakati ya maendeleo itakayoiwezesha Simba kupata mafanikio ya muda mrefu, badala ya kuangalia fedha pekee zitakazowekwa katika klabu.

Changawa pia anaeleza kuwa kuwa na wanachama wengi ni faida ambayo Simba inapaswa kuitumia kujenga mfumo imara wa kifedha na kibiashara.

Anasema tofauti kati ya klabu zinazofanikiwa na zinazokwama haipaswi kupimwa kwa kuangalia fedha pekee, bali pia ubora wa mipango, usimamizi wa rasilimali na uwezo wa viongozi kutekeleza mikakati ya maendeleo.

AATAKA SIMBA IWEKE MBELE MAFANIKIO

Changawa anasema mafanikio ya klabu hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wawekezaji au fedha zinazotajwa katika mipango ya uwekezaji pekee, bali kwa matokeo yanayoonekana katika maendeleo ya timu na uendeshaji wa klabu.

Amehoji mwenendo wa Simba katika mashindano, akisema ni muhimu kwa viongozi kueleza mikakati itakayoiwezesha timu kuwa na ushindani wa kudumu na kupata matokeo yanayotarajiwa na mashabiki wake.

Anasema klabu inahitaji mipango ya muda mrefu inayoweza kuleta utulivu katika uongozi, kuboresha maandalizi ya timu na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana zinatumika kwa ufanisi.

Changawa, anasema Simba ina wigo mkubwa wa mashabiki ambao unaweza kuwa msingi wa mafanikio ya kibiashara iwapo utawekewa mikakati madhubuti ya kuhamasisha ushiriki wao.

Amesisitiza kuwa wanachama wanapaswa kushirikishwa katika mijadala inayohusu klabu yao, huku viongozi wakitakiwa kuwajibika kwa maamuzi yanayofanywa kwa niaba ya taasisi hiyo.

MWITO WA KULINDA MASLAHI YA SIMBA

Changawa anasema kundi alilolitaja kuwa Linda Simba limeundwa kwa lengo la kutetea maslahi ya klabu na kuhimiza maamuzi yanayozingatia katiba, haki za wanachama na thamani ya taasisi hiyo.

Anasema jitihada za kulinda Simba hazipaswi kuchukuliwa kama upinzani dhidi ya mtu binafsi, bali kama sehemu ya mjadala mpana kuhusu namna ya kuhakikisha klabu inaendelea kuwa imara kiutawala na kiuchumi.

Anaeleza kuwa wanachama wanapaswa kuwa na nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu masuala yanayogusa umiliki, uwekezaji na uendeshaji wa klabu, huku taratibu rasmi zikifuatwa katika kufanya maamuzi.

Changawa amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa umoja, uwazi na uwajibikaji ndani ya Simba, akisema kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kulinda maslahi ya klabu na kuhakikisha inaendelea kuwa na ushindani katika soka la Tanzania na kimataifa.