Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Dickson Mollel, amesema uwepo wa Baraza la Wafanyakazi ni muhimu kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa mipango ya taasisi na kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake.Amesema hayo Oktoba 29, 2026 jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la PSPTB, akibainisha kuwa vikao hivyo husaidia kutathmini mipango iliyowekwa, hatua iliyofikiwa pamoja na namna ya kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji.

Aidha, Mollel amesema utekelezaji mzuri wa bajeti ya taasisi unatoa matumaini kwa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi kuwasilisha mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Ameongeza kuwa taasisi inapofanya vizuri katika utekelezaji wa bajeti, inakuwa na nafasi nzuri ya kuwasilisha na kutekeleza mawazo yanayolenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi, huku akieleza kuwa kutofanya vizuri kwa taasisi kunaweza kufanya suala hilo kuwa gumu.

Katika hatua nyingine, Dickson Mollel amesema ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti ni mkubwa, akibainisha kuwa kila idara katika taasisi inapata wawakilishi katika mchakato huo.

Pia ameongeza kuwa uongozi wa TUGHE unashirikishwa kikamilifu katika masuala hayo, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya chama cha wafanyakazi na uongozi wa taasisi unalenga kutatua changamoto na kuifanya taasisi kusonga mbele kwa pamoja.