Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiongoza Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiteta jambo na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Barani Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), Mhe. Mamadou Biteye, wakati akiongoza Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa taasisi hiyo uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Vihatarishi, wa Bodi ya Taasisi ya Kujenga Uwezo Barani Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), Bi. Rania Antonopoulou, baada ya Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa taasisi hiyo uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiagana na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Barani Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), Mhe. Mamadou Biteye, baada ya Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa taasisi hiyo uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (wanne kulia), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Ubunifu, Utafiti na Maendeleo, Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Evodius Kanyamyoga, na Mwambata Siasa, Ubalozi wa Tanzania, Nigeria, Bw. Allen Kuzilwa, baada ya Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Ujumbe wa Wataalam wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Cotonou, Benin)
……….
Na Farida Ramadhani, Cotonou, Benin
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inalenga kufanya umeme na nishati ya uhakika kuwa msingi wa mapinduzi ya uchumi yatakayochochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji, ajira na maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050, huku ikilenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030/31.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya kuongoza Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), unaofanyika sambamba na Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.
Mhe. Luswetula alisema Tanzania inatambua kuwa upatikanaji wa umeme na nishati ya uhakika ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi, hususan katika kuvutia uwekezaji, kupanua uzalishaji viwandani, kuimarisha miundombinu na kuboresha maisha ya wananchi.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa nishati ya kutosha ni miongoni mwa nguzo zitakazosaidia kufanikisha kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ya kufikia uchumi wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, na wastani wa pato la mtu mmoja kufikia takriban dola za Marekani 7,000.
“Tanzania tupo tayari kwa mapinduzi ya kiuchumi kwa sababu malengo yetu na nia yetu ni kuhakikisha tunakuwa na umeme na nishati ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, maendeleo ya Taifa na kukuza uchumi wetu,” alibainisha Mhe. Luswetula.
Alisema Serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo, yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kiuchumi, uwekezaji mpya na upanuzi wa viwanda nchini.
“Lengo letu ni kufikia zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030/31. Tunajua kuwa ili tuweze kuanzisha viwanda vingi, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi, ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,” alisema Mhe. Luswetula.
Alieleza kuwa upatikanaji wa umeme wa kutosha utawezesha kuanzishwa kwa viwanda vingi, kuongeza uzalishaji na kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), inayotarajiwa kufika Mwanza, Kigoma na maeneo mengine nchini.
Alibainisha kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika utasaidia kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wapya na waliopo kupanua shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi.
Mhe. Luswetula alisema kuwa sera zinazotekelezwa sasa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeendelea kuweka mazingira bora kwa wawekezaji na wafanyabiashara waliopo nchini, pamoja na wale wanaotaka kuwekeza kwa mara ya kwanza.
Mhe. Luswetula alisisitiza kuwa juhudi za Serikali hazilengi kuongeza uzalishaji wa umeme pekee, bali pia kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi na kuchangia maendeleo ya shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kupanua upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu, huku zaidi ya vitongoji 9,000 vipya vikitarajiwa kupata umeme katika awamu inayoendelea.
Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (ACBF) umejikita katika kujadili masuala ya nishati, kuanzia uzalishaji na usambazaji hadi kuhakikisha wananchi wananufaika na upatikanaji wa nishati hiyo.
Katika mkutano huo, Tanzania imejadiliana na washiriki kutoka nchi nyingine za Afrika kuhusu kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na utoshelevu wa nishati na kuanzisha viwanda vingi, huku umeme ukiwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika nchi hizo.
