Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Nguvila akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba jijini Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
ARUSHA: Wataalamu wa sayansi na teknolojia wametakiwa kuimarisha tafiti zinazolenga kupata suluhisho la changamoto za upatikanaji na usimamizi wa maji, huku mabadiliko ya tabianchi yakitajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayohitaji hatua za haraka ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa maisha na maendeleo ya kiuchumi.
Hayo yamesemwa jijiji Arusha na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Nguvila, aliyesisitiza kuwa usimamizi wa maji unapaswa kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika mazingira ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kupatikana kwa matumizi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Dk. Nguvila alitoa kauli hiyo jijini Arusha alipomwakilisha Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, katika ufunguzi wa kongamano la kisayansi la kikanda lililowakutanisha wadau kujadili namna ya kuboresha usimamizi wa maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika Afrika Mashariki na Kusini.
Amesema kuwa athari za tabianchi zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta zinazotegemea maji, zikiwemo kilimo na uzalishaji wa umeme, huku mafuriko na ukame vikiweza kuleta changamoto katika maisha ya wananchi na uendeshaji wa miundombinu.
Amesisitiza kuwa matumizi ya maarifa ya kisayansi katika kupanga na kusimamia rasilimali za maji ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mabadiliko ya mazingira, akitaja pia uhifadhi wa vyanzo vya maji kuwa eneo linalohitaji kupewa kipaumbele.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Profesa Maulilio Kipanyula, alisema maendeleo ya sayansi yanapaswa kupimwa kwa namna yanavyosaidia kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na kuboresha shughuli za uzalishaji.
Profesa Kipanyula, aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa tafiti zinazofanywa na wataalamu zinapaswa kuhusishwa na mahitaji halisi ya jamii ili matokeo yake yaweze kutumika katika kubuni teknolojia na mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za maendeleo.
Amebainisha pia kuwa kuandaa watafiti vijana ni sehemu muhimu ya kujenga uwezo wa Afrika katika sayansi na teknolojia, akihimiza uwekezaji utakaowawezesha kupata maarifa na ujuzi wa kubuni suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Zakia Meghji, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika tafiti na maamuzi yanayohusu usimamizi wa rasilimali za maji.
Amesema ushiriki wa wanawake katika matumizi ya teknolojia na tafiti za kisayansi unaweza kusaidia kupanua wigo wa mawazo na suluhisho zinazotumika kukabiliana na changamoto za maji, huku mahitaji ya makundi mbalimbali ya jamii yakizingatiwa katika mipango ya maendeleo.

