Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (MB), ameshiriki
Maadhimisho ya miaka 103 ya Jamhuri ya Uturuki yaliyofanyika jijini Dar es Salaan Oktoba 26,2026.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Dkt. Maghembe aliwasilisha pongezi na salamu za heri kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali na wananchi wa Tanzania, kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Serikali na wananchi wa Uturuki, katika kuadhimisha miaka 103 ya Jamhuri ya Uturuki, ambako huadhimishwa Oktoba 29 ya kila mwaka.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anaungana na wananchi wa Uturuki katika kusherehekea kuanzishwa kwa Jamhuri yao ya kisasa, hatua muhimu ya kihistoria inayodhihirisha mamlaka ya nchi hiyo, ustahimilivu, umoja wa kitaifa na dhamira endelevu ya kuendeleza amani, utulivu na ustawi,” alisema.
Alisema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari uhusiano wa muda mrefu na wa kirafiki kati ya Tanzania na Uturuki, ambao unaendelea kuimarika kupitia mazungumzo ya kidiplomasia, mashauriano ya kisiasa na ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Alisema Tanzania inasisitiza dhamira yake ya kuendeleza uhusiano wa pande mbili na kupanua wigo wa ushirikiano kwa manufaa ya Tanzania na Uturuki.
Aliongeza kuwa Tanzania na Uturuki zinatambua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kukuza uchumi, biashara na uwekezaji, elimu, afya, maendeleo ya miundombinu, utalii na mahusiano baina ya wananchi.
Alisisitiza Tanzania inathamini ushirikiano wake na Uturuki na inaendelea kujizatiti kutafuta fursa zaidi za ushirikiano zitakazonufaisha wananchi wa mataifa yote mawili.

