WAZIRI wa Afya,Mohamed Mchengerwa akifungua mkutano huo jijini Arusha leo

……….

Na Happy Lazaeo, Arusha 

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa amewataka vijana nchini kutumia fursa zilizopo katika sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa dawa, akisisitiza kuwa kujiajiri ni njia muhimu ya kujenga uchumi na kupunguza utegemezi wa ajira za serikali.

Ameyasema hayo jijini Arusha leo wakati akifungua Kongamano la kisayansi na mkutano mkuu wa 27 wa Chama cha Wateknolojia dawa Tanzania (TAPHATA) wenye kauli mbiu ya “kukuza viwanda vya dawa Tanzania kwa ajili ya Afya bora,ajira endelevu, na uchumi imara “.

Amesema serikali ipo tayari kushirikiana na wawekezaji wenye nia ya kuanzisha viwanda vya dawa nchini kwa kuwawekea mazingira wezeshi, ikiwemo mikataba ya makubaliano (MoU) inayoweza kusaidia kupata mitaji kutoka taasisi za kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi yao.

Mchengerwa amesema kuwa kupitia mikataba hiyo, serikali inaweza kuonesha dhamira ya kununua dawa zitakazozalishwa na viwanda vya ndani, endapo zitakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa. Hali hiyo inaweza kuwapa wawekezaji uhakika wa soko na kuwasaidia kupata fedha za kuanzisha au kupanua biashara zao.

Aidha amewahimiza vijana kuondokana na fikra kwamba mafanikio ya maisha yanategemea kuajiriwa pekee, akibainisha kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi na kutoa ajira. Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kutumia fursa hizo badala ya kuziachia kampuni za kigeni pekee.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sifa za kitaaluma kwa wanaotaka kujiunga na fani za udaktari na famasia, akieleza kuwa masomo ya sayansi, yakiwemo kemia, fizikia na hisabati, yana nafasi muhimu katika kuwaandaa wataalamu wenye uwezo wa kutengeneza na kusimamia matumizi sahihi ya dawa.

“Wataalamu wa famasia wana jukumu muhimu katika mfumo wa afya, ikiwemo kutoa ushauri kuhusu dawa zinazofaa kutumika pale dawa fulani inapokosekana. Kwa sababu hiyo, amesema ni muhimu kuhakikisha wanaojiunga na fani hiyo wana maarifa na uwezo unaohitajika ili kulinda usalama wa wagonjwa.”amesema Mchengerwa.

Aidha ametoa wito kwa Wizara ya Elimu na wadau wa sekta ya dawa kushirikiana kuboresha mitaala ya mafunzo ili kuandaa vijana wenye ujuzi wa kutengeneza dawa na kushiriki katika shughuli za usajili na uzalishaji wa bidhaa za dawa nchini.

“Tanzania inahitaji kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha dawa kwa kuimarisha ujuzi wa wataalamu, tafiti na uwekezaji katika viwanda. “amesema .

Ameonya kuwa ubora wa elimu na mafunzo ya kitaaluma haupaswi kushushwa kwa lengo la kupata fedha, akisisitiza kuwa viwango vinavyowekwa vinapaswa kulinda ubora na weledi wa wataalamu.

Waziri huyo amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuboresha ushirikiano kati ya wazalishaji wa dawa na mamlaka za udhibiti ili kuhakikisha taratibu za usajili na uzalishaji zinafuatwa, huku bidhaa zinazozalishwa zikikidhi viwango vinavyotakiwa na kusaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini.