NA DENIS MLOWE, IRINGA

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Vijana, Jasmin Ng’umbi, ameitoa wito kwa Serikali kuimarisha mchezo wa pete nchini kwa kuweka mfumo wa mashindano wenye madaraja mbalimbali na ligi za kudumu ili kuongeza ushindani, kuibua vipaji na kurejesha mvuto wa mchezo huo.

Ng’umbi ametoa hoja hiyo Bungeni akitaka Serikali kueleza mipango yake ya kusaidia maendeleo ya mchezo huo, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa Chama cha Mpira wa Pete Tanzania (CHANETA) ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema mchezo wa pete una mashabiki wengi nchini na una uwezo wa kukua zaidi endapo kutakuwa na mfumo madhubuti wa mashindano, utakaowezesha timu kushindana katika madaraja tofauti kama ilivyo katika mchezo wa mpira wa miguu.

Jasmine amesisitiza umuhimu wa kuwa na ligi na mashindano ya mara kwa mara yatakayowapa wachezaji nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, kuongeza ushindani na kuimarisha hadhi ya mchezo huo nchini.

Akijibu maswali yaliyoulizwa na Ng’umbi, Naibu Waziri wa michezo. Hamis Mwinjuma amepongeza juhudi za mbunge huyo katika kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mchezo wa pete ndani na nje ya Bunge.

Amesema Ng’umbi amekuwa akifuatilia masuala ya mchezo huo na kuwasilisha hoja mbalimbali zinazolenga kuimarisha maendeleo yake, jambo linaloonyesha dhamira yake ya kuona mchezo huo unarejesha mvuto na hadhi iliyokuwa nayo.

Kuhusu ombi la Serikali kusaidia CHANETA ili kupata uthamini na kuimarisha uendeshaji wa mchezo huo, Naibu Waziri Hamis Mwinjuma amesema Serikali inaendelea na mipango ya kuimarisha uongozi na kuboresha misingi ya utawala bora ndani ya chama hicho, ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikikabiliwa na changamoto za kiutawala.

Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira bora ya usimamizi wa chama na kuwezesha mchezo wa pete kuendelea kukua, huku wadau wakitarajia kuona mfumo wa mashindano unaoongeza ushindani na kuwapa wachezaji fursa zaidi za kuendeleza vipaji vyao