Zoezi la utoaji elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki limefanyika rasmi Oktoba 26, 2026, katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Zoezi hilo ni sehemu ya mchakato wa kuwajengea wananchi uelewa kuhusu rasimu hiyo na kukusanya maoni yatakayochangia kuandaa Katiba itakayoimarisha mtangamano wa kikanda.

Akifungua zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewahimiza wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao. Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuamua mustakabali wa ukanda huo.

Zoezi hilo limewakutanisha viongozi wa serikali za mikoa na wilaya, wajumbe wa kamati za usalama na siasa, wakurugenzi, taasisi za dini, Benki Kuu ya Tanzania, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia. Vile vile makundi ya vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na wawakilishi wa vyuo vikuu.

Akiwasilisha mada, Mjumbe wa Kamati ya Afrika Mashariki ya Ukusanyaji wa Maoni ya wananchi na Uandishi wa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki kutokea Tanzania Dkt. Idd Mandi, ameeleza kuwa Fungamano la Kisiasa ni hatua ya mpito kuelekea Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, lililopitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC mwaka 2017. Amesema fungamano hilo halimaanishi nchi kupoteza uhuru na mamlaka ya kitaifa, bali kushirikiana kwa karibu katika maeneo ya kimkakati kwa manufaa ya wananchi.

Dkt Mandi amefafanua maeneo yanayohitaji maoni ya wananchi kuwa muundo wa utawala, mfumo wa kufanya maamuzi, maeneo ya ushirikiano, uhusiano kati ya serikali za nchi wanachama na mamlaka ya fungamano, pamoja na namna ya kugharamia shughuli zake.

Kwa upande wa washiriki walipata fursa ya Kufanya mjadala na kuuliza maswali kuhusu Fungamano hilo. Hatua hii ni sehemu muhimu ya juhudi za Jumuiya ya Afrika Mashariki za kuwashirikisha wananchi katika kuandaa katiba itakayoweka misingi ya ushirikiano wa kisiasa na kuimarisha mtangamano wa kikanda.