Na Meleka Kulwa– Fullshangwe Blog, Dodoma

MAMLAKA Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma a (DUWASA) imepanga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 91 kwa siku hadi lita milioni 121 kwa siku, ikiwa ni sehemu ya mpango wa miaka mitano wa kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Dodoma.Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 26, 2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya hali ya huduma ya majisafi, utekelezaji wa miradi na uharibifu wa miundombinu ya DUWASA, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema kwa sasa mahitaji ya maji jijini Dodoma ni lita milioni 159.9 kwa siku, wakati uwezo wa uzalishaji ukiwa lita milioni 91 kwa siku.

Amesema hali hiyo imeifanya DUWASA kuzalisha takribani asilimia 57 ya mahitaji ya maji kwa siku, jambo linalosababisha kuwepo kwa mgawo wa maji, huku mahitaji yakitarajiwa kufikia lita milioni 180 kwa siku ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amebainisha kuwa DUWASA imeandaa mpango mkakati na mpango wa biashara wa miaka mitano unaolenga kuongeza uzalishaji wa maji hadi lita milioni 121 kwa siku, ambapo miradi iliyokwishaandaliwa na mingine iliyoanza kutekelezwa ina thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 51.

Pia ameongeza kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa kuongeza huduma ya maji katika Mji wa Serikali wenye thamani ya Shilingi bilioni 35, unaohusisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa matanki yenye uwezo wa Zaidi ya lita milioni sita pamoja na ujenzi wa mtandao wa kusafirisha na kusambaza maji wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60, kwa lengo la kuhudumia Mji wa Serikali na maeneo yanayouzunguka