Na Mwandishi Wetu, Korogwe
WANANCHI wa Kijiji cha Vuje, kilichopo Kata ya Bungu Korogwe Vijijini, wameingia kwenye furaha kubwa baada ya kushuhudia mkandarasi akabidhiwa rasmi mradi wa maji wa shilingi milioni 107.65 utakaokomesha adha ya ukosefu wa huduma hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miongo mitano tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1972.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi katika hafla hiyo ya kihistoria iliyovuta hisia za wengi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vuje, Muhammad Dhahabu, alieleza namna jamii ilivyoteseka kwa muda mrefu kusaka maji na kupoteza imani kutokana na ahadi za mara kwa mara zilizokosa utekelezaji, akimshukuru Mbunge wa Jimbo, Timotheo Mnzava, kwa kuwatendea haki.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bungu, Stephen Mdoe, licha ya kuishukuru serikali kwa uamuzi huo wa kishujaa, aliwasilisha kilio cha wananchi kuhusiana na uhaba wa maeneo ya kilimo kufuatia mashamba ya chai yaliyozunguka kijiji hicho kutelekezwa na wakulima kupigwa marufuku kuyatumia kwa mazao ya muda mfupi kama mahindi na magimbi.
Akiweka wazi takwimu za mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe, Muharami K. Mohamedi, alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kizalendo ya Amani Civil and Water Works, ukilenga kuwanufaisha wakazi 1,297 kupitia ukarabati wa banio huko Sakale, matanki ya maji, na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 4.5 kwa kipindi cha miezi mitatu.
Akihutubia kwa niaba ya Mbunge Mnzava, mwakilishi wake Shebila Idd — ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira — alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowawezesha wakazi wa Vuje kulala kwa amani, huku wananchi wakicheza na kuimba nyimbo za kumsifu kiongozi huyo mkuu wa nchi.
“Rais Samia amedhihirisha kuwa yeye ni daktari wa kutatua na kutibu changamoto mbalimbali zinazotukabili sisi wananchi, hakika ni mama msikivu sana,” alisema Shebila.
Shebila aliwataka wananchi wa Korogwe kuendelea kumlinda na kumuunga mkono Mbunge Mnzava, akisisitiza kuwa amefanya makubwa yaliyowashinda watangulizi wake katika sekta za maji, umeme, barabara, afya na elimu, jambo linalofanya jimbo hilo kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Mheshimiwa Mnzava ni mbunge tunatakiwa tumlinde, asituponyoke, tumuunge mkono, kazi zetu tunazomtuma anazifanya, waliomtangulia hawakuwa na Kasi kama yake,” alisema Shebila.
Akizungumza kwa njia ya simu na wananchi hao, Mbunge Timotheo Mnzava alisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni uthibitisho tosha wa namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotatua kero za wananchi kwa vitendo.
“Leo (Oktoba 25, 2026), tumefanya jambo kubwa na la kipekee kukabidhi mradi huu wa maji, tumshukuru sana mhe Rais kwa anajali matatizo ya wananchi wake,” alisema.
Mnzava alisema alipofika katika Kijiji hicho alipopewa kero ya maji hakuwa akipata usingizi na anamshukuru Rais kumpatia fedha ambazo zimeweza kutimiza ahadi yake.
Mnzava alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa pamoja na diwani na Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambaye alikuwa akifuatilia kuona fedha zinapatikana ili wananchi waondokane na kero hiyo.
Mbunge huyo aliwataka wakazi wa Vuje kushirikiana kwa karibu na mkandarasi ili kazi ikamilike kwa ubora uliokusudiwa

