LINDI, OKTOBA 26, 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema Serikali inaendelea na hatua za kuhakikisha Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kuwa Gesi Asilia Kimiminika (LNG) unaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo, huku ikihakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa.

Dkt. Mataragio ameyasema hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati wa uzinduzi wa Shule ya Awali na Msingi Likong’o, iliyojengwa kwa ushirikiano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wawekezaji wa mradi huo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), mkoani Lindi.

Amesema Serikali inaendelea na majadiliano kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa mradi huo unapoanza kutekelezwa unaleta manufaa kwa wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla, bila kuathiri maslahi ya taifa.

Ameeleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika majadiliano kuhusu masuala muhimu ya mradi, yakiwemo biashara na kodi, huku suala la sheria maalumu ya mradi likiwa miongoni mwa hatua zilizobaki kukamilishwa.

Amesema majadiliano kuhusu suala hilo yanatarajiwa kuendelea hivi karibuni jijini Arusha, kwa lengo la kuweka mfumo wa kisheria utakaolinda maslahi ya taifa, wananchi na wawekezaji.

Dkt. Mataragio ameeleza kuwa sheria hiyo maalumu inatarajiwa kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi kilichopangwa cha miaka 50.

Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha kuwa makubaliano ya mradi yanazingatia maslahi mapana ya wananchi wa Lindi na Watanzania wote, sambamba na kuweka mazingira ya usalama na uhakika kwa wawekezaji.

Amewataka wananchi kuwa na subira, akieleza kuwa Serikali inaendelea na hatua muhimu za kukamilisha majadiliano ili kufikia hatua ya kusaini mikataba na kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Dkt. Mataragio amewashukuru wawekezaji wa Mradi wa LNG kwa kushirikiana na TPDC kujenga Shule ya Awali na Msingi Likong’o kupitia mpango wa CSR, akibainisha kuwa hatua hiyo ni mchango muhimu kwa jamii hata kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa LNG.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mataragio ametangaza ratiba ya shughuli za Wiki ya Mafuta na Gesi, ambapo kesho, Oktoba 27, 2026, Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, anatarajiwa kuwa mkoani Mtwara kutangaza ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia.

Ameeleza kuwa Oktoba 28, 2026, kutakuwa na hafla ya kukabidhi leseni za uchimbaji na uendelezaji wa visima kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.