Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imebaini wizi wa mita 103 za maji ndani ya kipindi cha miezi mitatu, huku ikiwataka wananchi kushirikiana na mamlaka hiyo kulinda miundombinu ya huduma za maji na majitaka jijini Dodoma.Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema hayo Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo, ikiwemo wizi wa mita za maji na mifuniko ya chemba za majitaka.

Amesema wizi wa miundombinu hiyo unaweza kuongeza gharama za uendeshaji na kuhatarisha usalama wa wananchi, hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya wizi au watu wanaoshukiwa kujihusisha na uharibifu wa miundombinu.

Aidha,amesema Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019 pamoja na Kanuni ya 47 inaelekeza mita za maji kufungwa nje ya geti au fensi kwa kushirikiana na mteja, ili kurahisisha usomaji na uhakiki wa mita hizo.

Amesema pamoja na utaratibu huo, takribani asilimia 70 ya wateja wa DUWASA jijini Dodoma wana mita zilizofungwa ndani ya fensi, hali inayoweza kuleta changamoto wakati wa usomaji wa mita kila mwezi.

Pia amewataka wateja wenye mita zilizofungwa ndani ya fensi kushirikiana na DUWASA kuhakikisha usomaji unafanyika kwa wakati, huku akisisitiza kuwa hakuna mteja anayepaswa kuhamisha au kuingilia mita bila kushirikisha mamlaka hiyo ili kuepusha hitilafu.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Aron amekemea wizi wa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka, akisema kuondolewa kwake kunaweza kuacha chemba wazi na kuhatarisha usalama wa watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na madereva.

Amesema baadhi ya mifuniko hiyo ina alama za DUWASA na imetengenezwa kwa chuma kizito ili kuhimili uzito wa magari makubwa yanayopita barabarani, hivyo wananchi hawapaswi kupokea wala kununua mifuniko hiyo kutoka kwa watu wanaoshukiwa kuwa wezi.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kutumia namba rasmi za dharura za DUWASA wanapobaini wizi wa mita za maji au mifuniko ya chemba za majitaka, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda miundombinu na kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira jijini Dodoma.