Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

Serikali imewataka vijana nchini kutumia mitandao ya kijamii kujifunza, kutafuta masoko ya bidhaa zao, kufanya ubunifu na kutengeneza fursa za kiuchumi badala ya kuitumia kuhamasisha vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 25, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa vijana ndio watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikitumika kuhamasisha vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Amesema kuwa vijana wanapaswa kuwa makini na mambo yanayoendelea mitandaoni, akibainisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafuatilia vitendo vya uchochezi vinavyofanyika kupitia mitandao hiyo.

Aidha, amewataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza pesa, kujifunza, kutafuta masoko ya bidhaa zao, kufanya ubunifu, kupata burudani na kutengeneza connections za kupata fursa za kiuchumi.

Pia ameongeza kuwa hakuna aliyefanikiwa kwa kushiriki katika uharibifu na kwamba kufanya uharibifu ni kujiharibia maisha.

Huku akibainisha kuwa madai ya wananchi yapo na mifumo ya Serikali ipo kwa ajili ya kushughulikia madai hayo kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo nchini.

Amesema kuwa madai mbalimbali ya wananchi hayatatuliwi kwa vurugu, kuchocheana, kutiana hasira na kuharibu misingi ya nchi, bali yanapaswa kufanyiwa kazi kupitia mifumo iliyopo.

Aidha, amewataka Watanzania wote kukataa hamasa zinazolenga kuwashawishi kushiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria na kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi.

Pia amebainisha kuwa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama vipo imara kuhakikisha vinasimamia amani na usalama wa watu na mali zao pamoja na usalama wa mipaka ya nchi.

Amesema kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba yeyote atakayevunja sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Pia ameongeza kuwa Tanzania inahitaji amani na utulivu ili iweze kuelekeza nguvu katika uzalishaji, biashara, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuinua ustawi wa jamii.