Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa Sh. bilioni 730 zilizotajwa katika Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño si bajeti mpya iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na mvua hizo, bali ni jumla ya makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutoka taasisi mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 25, 2026, amesema kuwa kiasi hicho kinajumuisha bajeti na rasilimali za taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali zinazohusika katika utekelezaji wa mpango huo, huku kila taasisi ikitumia rasilimali zilizopo ndani ya bajeti zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amebainisha kuwa mpango huo umeandaliwa kufuatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu, ambayo inaweza kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko, uharibifu wa makazi na miundombinu pamoja na hasara za kiuchumi na kijamii.
Pia ameongeza kuwa mpango huo unahusisha hatua mbalimbali ikiwemo ukarabati wa barabara, madaraja na mitaro katika maeneo hatarishi, kuhakikisha huduma za afya, elimu, maji, umeme na mawasiliano zinaendelea, pamoja na kuimarisha akiba ya chakula na maandalizi ya vifaa vya uokoaji na misaada ya kibinadamu.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za tahadhari za mapema zinazotolewa na TMA na mamlaka nyingine husika ili waweze kuchukua hatua kwa wakati, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo unahusisha Serikali, Serikali za Mitaa, mashirika ya kitaifa na kimataifa, sekta binafsi na wadau wengine.
