TUNDURU
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amewasha umeme katika Kitongoji cha Nakanyonyo, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme na kutumia nishati hiyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mradi wa kupeleka umeme katika Kitongoji cha Nakanyonyo umetumia Shilingi 82.86 milioni na ulihusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo mdogo yenye urefu wa kilomita 1.889, ufungaji wa mashineumba moja yenye uwezo wa KVA 100, pamoja na kuunganisha wateja.
Jimbo la Tunduru Kaskazini lina jumla ya vijiji 92, ambavyo vyote vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Kati ya vitongoji 602 vilivyopo jimboni humo, vitongoji 482 tayari vimefikiwa na umeme, huku vitongoji 99 vikiwa katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
Miradi hiyo ikikamilika, jumla ya vitongoji 581 vitakuwa vimefikiwa na umeme, sawa na asilimia 97 ya vitongoji vyote vya jimbo hilo. Vitongoji 21 vilivyosalia vipo katika hatua za kuingizwa kwenye miradi itakayoanza kutekelezwa hivi karibuni.
Kwa upande wa Kata ya Nakayaya, vijiji vyote vitano vimefikiwa na miundombinu ya umeme, huku vitongoji vyote 20 vya kata hiyo vikiwa vimefikiwa na umeme, sawa na asilimia 100.
Upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi, kurahisisha shughuli za kijamii na kuwawezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.

