Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepokea vyeti vya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora kwa mujibu wa kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 kwa ofisi zake nane, ikiwemo Makao Makuu, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi, uwazi, uwajibikaji na ubora wa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vyeti hivyo iliyofanyika Dar es Salaam, Oktoba 21, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema kupata vyeti hivyo ni hatua muhimu katika kuboresha mifumo na taratibu za kazi za taasisi hiyo, hususan katika upokeaji na ushughulikiaji wa maombi ya mikopo, utoaji wa taarifa na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Amesema HESLB itaendelea kuimarisha mifumo yake ya kiutendaji na kiteknolojia ili kuhakikisha wanafunzi wanufaika wa mikopo na ruzuku wanapata huduma zenye ufanisi, zinazotolewa kwa wakati na zinazokidhi mahitaji yao pamoja na matarajio ya wazazi, walezi, taasisi za elimu ya juu na wadau wengine.
Dkt. Kiwia amesisitiza kuwa kupokea vyeti hivyo si mwisho wa safari ya kuboresha huduma, bali ni mwanzo wa kuendeleza utamaduni wa ubora katika shughuli za kila siku za taasisi hiyo, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, kufuatilia matokeo na kufanya maboresho endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema ISO 9001:2015 ni kiwango cha kimataifa kinachoiwezesha taasisi kuweka na kutekeleza mifumo madhubuti ya kusimamia ubora wa huduma, kuongeza ufanisi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji na matarajio ya wateja na wadau.
Dkt. Katunzi amesema makabidhiano ya vyeti hivyo kwa HESLB ni hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya utoaji huduma na kusisitiza umuhimu wa taasisi kuendelea kuzingatia matakwa ya kiwango hicho ili manufaa yake yaonekane katika utendaji wa kila siku.
Ameeleza kuwa mfumo wa usimamizi wa ubora unasaidia taasisi kuweka taratibu za kazi zilizo wazi, kutambua maeneo yanayohitaji maboresho, kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Amesisitiza kuwa kupata cheti cha ISO 9001:2015 kunahitaji taasisi kuendelea kudumisha viwango vya ubora, kufuatilia utekelezaji wa mifumo yake na kufanya maboresho yanayolenga kuongeza ufanisi na kuridhika kwa wateja.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kazi ya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa HESLB, Bwana Bahati Singa, amesema safari ya kuandaa na kutekeleza mfumo huo ilianza Machi 2025 kwa kuzingatia maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu wa HESLB na dhamira ya kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na bodi hiyo.
Amesema katika hatua za awali, HESLB ilifanya mapitio ya michakato ya kazi, kubainisha maeneo yaliyohitaji maboresho na kuweka taratibu zilizo wazi, zinazotekelezeka na zinazoweza kupimwa ili kuhakikisha shughuli za taasisi zinaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya mfumo wa usimamizi wa ubora.
Bwana Singa amesema kwa mwongozo wa kitaalamu kutoka TBS, Februari 2026 HESLB ilifanya mafunzo ya utekelezaji wa mfumo huo na kuandaa nyaraka zinazohitajika, huku idara na vitengo vikishirikiana kuboresha taratibu za kazi na kuweka malengo ya ubora.
Ameongeza kuwa Aprili 2026, bodi hiyo ilifanya ukaguzi wa ndani na mapitio ya menejimenti ili kutathmini utekelezaji wa mfumo, kubaini changamoto na kuelekeza maboresho yaliyohitajika, kabla ya kuendelea na hatua za uthibitishaji zilizofanyika Mei na Juni 2026.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa menejimenti, watumishi wa HESLB na wataalamu wa TBS, akiwapongeza Mabingwa wa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS Champions) na Mratibu wa mfumo huo, Ninkambazi Muze, kwa mchango wao katika kuhakikisha taasisi inakidhi vigezo vya kupata uthibitisho huo.
Bwana Singa amehitimisha kwa kusema Kamati ya Kazi ya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora itaendelea kushirikiana na menejimenti pamoja na watumishi wa HESLB kuhakikisha viwango vilivyothibitishwa vinadumishwa, changamoto zinashughulikiwa kwa wakati na mrejesho wa wateja unazingatiwa ili kuboresha huduma kwa wanafunzi na wadau wengine.
ISO 9001:2015 ni kiwango cha kimataifa kinachoweka matakwa ya mfumo wa usimamizi wa ubora, kikilenga kuboresha michakato ya kazi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi zinaendelea kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja na kufanya maboresho endelevu.

