Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuzipatia ufumbuzi kwa wakati changamoto za majenzi nchini ili kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Akifungua Mkutano mkuu wa sita wa mwaka wa AQRB jijini Arusha leo Eng. Kasekenya amesisitiza wataalam wa Serikali katika sekta ya ujenzi kuondoa urasimu na kuongeza ubunifu ili kuiwezesha sekta binafsi nchini kukua na kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.

” Hakikisheni mnazibaini changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati kwa kuandaa mipango na mikakati inayotekelezeka na kupimika”, amesisitiza Eng. Kasekenya.

Amesema Serikali italifanyia kazi pendekezo la AQRB la kuwa na mradi mmoja, namba moja ya utambulisho na mfumo mmoja wa ufutiliaji ili kuleta tija katika shughuli za ujenzi nchini.

Naibu Waziri Kasekenya amesema Wizara ya ujenzi na taasisi zake ziimarishe uratibu wa usajili, vibali vya ukaguzi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote ya ujenzi nchini inazingatia sheria na kulinda usalama wa watu na mali.

Wizara ya Ujenzi itahakikisha inafanya tathmini na uchambuzi wa kina ili kuhakikisha sheria jumuishi ya majengo inalinda usalama wa wananchi bila kuathiri ukuaji wa sekta ya ujenzi na maendeleo kwa ujumla

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Neema Lugangira amezungumzia umuhimu wa kuwa na sheria mahsusi ya majengo na kuhakikisha watanzania wananufaika na miradi mikubwa ya ujenzi nchini.

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Arch. Daniel Matondo amesema Bodi hiyo imejipanga kukua na kuendana na Dira ya Maendeleo 2050.

” Ninachokibuni, ninachokikadiria kilete tija ya kiusalama, kiuchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla”, amesema Arch. Matondo.

Zaidi ya Wataalam 2185 wa ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi wamesajiliwa na AQRB tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997.

Arch. Matondo ameiomba Serikali kuanda sheria jumuishi ya majengo itakayoondoa muingiliano wa majukumu kwenye sekta ya ujenzi na kuchochea fursa za wazawa kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya ujenzi.

Mkutano huo wa sita umeongozwa na kaulimbiu isemayo; kuijenga Tanzania tunayoitaka kuelekea 2050: kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa mazingira endelevu ya ujenzi.