Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKURUGENZI wa shule ya awali na msingi Glisten iliyopo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Justin Nyari amewaasa wahitimu wa darasa la saba kuwa huo siyo mwisho wa elimu yao ila ni mwanzo wa safari yao.
Nyari ameeleza hayo kwenye tafrija ya mahafali ya sita ya shule ya awali na msingi Glisten yaliyofanyika hivi karibuni shuleni hapo katika taarifa yake kwa wahitimu hao.
Katika taarifa yake iliyosomwa na mwalimu wa shule hiyo, Diana Akama amesema baada ya kuhitimu darasa la saba wanakwenda kuanza maisha mapya shule ya sekondari.
“Leo ni siku ya furaha na fahari lakini kumbukeni kuhitimu darasa la saba siyo mwisho wa elimu yenu, ni mwanzo wa sura mpya, shule ya sekondari mtakutana na mazingira mapya, marafiki wapya na majukumu makubwa zaidi,” amesema Nyari.
Amewaasa wafanye maamuzi ya busara, wachague marafiki wema, wawasikilize wazazi na walimu wao na waiweke elimu mbele daima.
“Epukeni makundi mabaya, utoro, udanganyifu, matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya, mahusiano yasiyofaa na tabia yoyote inayoweza kuharibu maisha yenu ya baadaye,” amesema Nyari.
Amewahimiza wasikubali kamwe kushinikizwa na marafiki kutenda mabaya kwa sababu tu wengine wanafanya hivyo, wajifunze kusema hapana kwa jambo linalopingana na maadili na malengo yao.
Hata hivyo, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyojali na kuwekeza kwenye elimu ya watoto wa kitanzania.
“Tunaishukuru Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na watangulizi wake kwa kupanua fursa ya elimu kupitia elimu bila malipo na nafasi za kujiunga na shule za sekondari, tunamuomba Mungu azidi kumbariki Rais wetu, viongozi wetu na Taifa letu ili amani, umoja na maendeleo viendelee kuwepo,” amesema Nyari.
Amewatakia wahitimu kila la heri katika masomo yao ya sekondari na katika shughuli zao zote za baadaye Mungu awaongoze, awalinde na awape hekima ya kufanya maamuzi sahihi.
“Mnapoondoka Glisten, nendeni na shukrani, nidhamu, uadilifu na azma, kumbukeni shule yenu, walimu wenu na misingi mizuri mliyofundishwa, tunatarajia kuwaona mkifanya vizuri na kuwa raia wawajibikaji, wenye heshima na wenye tija,” amesema Nyari.
Amewashukuru wazazi na walezi wao kwa kuwaamini na kuwakabidhi watoto wao na kushirikiana nao katika malezi yao, walimu na wafanyakazi wao, anawashukuru kwa kujitoa kwao, uvumilivu wao na mchango wao katika ukuaji wa kitaaluma na kimaadili wa wanafunzi wao.
