Na Mwandishi Wetu, Tunduru
MNADA wa kwanza wa zao la korosho kwa Mkoa wa Ruvuma msimu 2026/2027,utafanyika kesho Oktoba 20 2026 huku uzalishaji ukitarajiwa kuongezeka kutoka tani 40,000 msimu 2025/2026 hadi tani 45,000 msimu 2026/2027.
Awali, mnada huo ulitakiwa kufanyika wiki iliyopita tarehe 13 Oktoba 2026, lakini ulishindwa kufanyika kutokana na changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru (Tamcu)kinachohudumia wakulima wa korosho wa mikoa ya Mbeya,Njombe na Ruvuma Mussa Manjaule alisema,mnada huo utafanyika katika viwanja vya Baraza la Idd Tunduru mjini.
Manjaule ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Korosho Tanzania(CBT),amewataka wakulima kupeleka korosho zenye ubora katika mnada wa kwanza ili wapate bei nzuri sokoni badala ya kusubiri minada inayofuata.
“Kwa sasa tunaendelea vizuri na makusanyo ya korosho kutoka kwa wakulima,tunaamini kwamba msimu huu tutavuka malengo tuliyojiwekea,nawaomba sana wakulima waendelee kupeleka korosho kwenye maghala yalivyopo kwenye maeneo yao”alisema Manjaule.
Amewasisitiza wakulima kuepuka kuchanganya korosho zilizokauka na zenye unyevu,kwani kufanya hivyo kunaweza kuathiri ubora na soko la uhakika.
Manjaule alisema,maandalizi yote yamekamilika ikiwemo kupeleka magunia na mahitaji mengine kama kamba na jumla ya maghala sita yameandaliwa ili kupokea korosho kutoka kwenye vyama vya msingi vya ushirika.
Alisema,makarani na watendaji wa vyama vya msingi vya msingi vya ushirika wamepata mafunzo namna ya kuwahudumia wakulima, kukusanya korosho huku akiwataka wakulima kufika kwa wingi katika mnada huo ili kushuhudia uuzaji wa korosho kupitia mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania(TMX).
Katika hatua nyingine,Manjaule amewasisitiza wakulima waendelee kukusanya korosho na kuzipeleka kwenye maghala,badala ya kuhifadhi majumbani ambako siyo sehemu sahihi na salama kutokana na changamoto zinazoweza kujitokea ikiwemo tishio la mvua za El-nino.
Alisema,korosho zinatakiwa kuanikwa kwa siku tatu hadi nne ili ziweze kukauka vizuri na ambazo hazijakauka au zenye unyevu zisipelekwe kwenye maghala ili kuepuka usumbufu.
Naye Meneja Mkuu wa Tamcu Marcelino Mrope alisema,kwa msimu 2026/2027 Chama hicho inatarajiwa kukusanya zaidi ya tani 45,000 sawa na kilo milioni 45 ikilinganishwa na tani 40,000 za msimu 2025/2026.
“Katika msimu 2026/2027 tumepanga kukusanya korosho tani 45,000 nawaomba wakulima wetu wazingatie ubora pamoja na kuhakikisha kuwa korosho zinaandaliwa na kukaushwa vizuri ili tuweze kuzipeleka kwenye maghala na kupata bei nzuri”alisema Mrope.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma Venance Msafiri,amewahakikishia wakulima wa korosho kwamba hakutakuwa na changamoto ya malipo kwenye zao hilo na amewapongeza watendaji wa Amcos kuwalipa wakulima fedha za mbaazi na ufuta katika msimu wa kilimo 2025/2026.
Alisema,Serikali kupitia vyama vya ushirika,itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya mizani za Kidijitali huku akiwasisitiza viongozi wa Amcos kuhakikisha matumizi ya mizani hizo kwenye ununuzi wa korosho na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
