Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewataka Watanzania kuthamini juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza miradi ya kimkakati, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili miradi hiyo ilete manufaa kwa Taifa.

Makamu wa Rais ametoa wito huo mkoani Iringa alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 41.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha usafiri wa anga, kufungua fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Aidha, amezitaka Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutathmini uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kiwanja hicho, ikiwemo kuweka taa zitakazowezesha ndege kutua na kuruka wakati wa usiku.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka Watanzania kuungana na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa kwa kutambua wajibu wao, badala ya kujiuliza Serikali imewafanyia nini. Amesisitiza kuwa kila Mtanzania anapaswa kujiuliza amelifanyia nini Taifa lake.

Amesema uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii ni miongoni mwa misingi muhimu ya kuongeza tija, kukuza mapato ya Serikali na kuboresha huduma za kijamii pamoja na miundombinu ya maendeleo.

Akizungumzia usimamizi wa fedha za umma, amewataka mawaziri, viongozi wa taasisi, wabunge, wakuu wa wilaya, madiwani na watendaji wa Serikali katika ngazi zote kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupambana na ubadhirifu pamoja na rushwa.

Ameonya dhidi ya watu wanaodai asilimia ya fedha za miradi bila kufanya kazi yoyote, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, haitawavumilia wabadhirifu na itahakikisha fedha za walipakodi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, amesema Serikali imetenga takribani shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songea, Sumbawanga, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Tanga, Mtwara, Lindi na Dodoma.

Amesema miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ambapo baadhi imekamilika, mingine inaendelea kujengwa, huku mingine ikiwa katika hatua za maandalizi ya ujenzi na taratibu za zabuni.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, akizungumzia kuchelewa kwa ujenzi wa barabara ya mchepuko ya Iringa, amesema mkandarasi aliyelipwa fedha za awali kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 3.3 aliondoka eneo la mradi na kusababisha kazi kusimama.

Amesema tayari ameitisha kikao na mkandarasi huyo ili kuhakikisha anarejea eneo la mradi na kuendelea na kazi. Aidha, amewaonya wakandarasi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa usajili na kuzuiwa kutekeleza miradi nchini.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 41 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2027.

Amesema mradi huo ulianza Julai 17, 2025, na unatekelezwa na kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited. Kwa sasa, kazi za ujenzi wa jengo la abiria na barabara za ndani zinaendelea.

Besta amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 140 kwa wakati mmoja, sawa na abiria 250,000 kwa mwaka, huku maegesho yake yakiwa na uwezo wa kuhifadhi magari 80. Miundombinu hiyo inatarajiwa kuchochea biashara, uwekezaji na utalii katika Mkoa wa Iringa na maeneo jirani.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema amemtaka Waziri wa Ujenzi kufanya mazungumzo na wakandarasi wanaotekeleza mradi wa barabara ya mchepuko (bypass) ya kuingia na kutoka Iringa Mjini ili kufikia mwafaka utakaowezesha ujenzi kukamilika, ikizingatiwa kuwa Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya mradi huo.