Na Ashrack Miraji , Same
Katika kuchukua hatua madhubuti za kulinda usalama wa wananchi, kudhibiti uhalifu, na kukata mzizi wa fitina wa ajali za barabarani zinazoweza kuzuilika, Jeshi la Polisi wilayani Same limeanza rasmi kampeni kabambe ya “Ongea na Kamanda” inayolenga kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 18, 2026 na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Same, SSP Tom Obonyo, wakati akizungumza ana kwa ana na waendesha bodaboda pamoja na mawakala wa mabasi katika Stendi Kuu ya Same, akiwakumbusha wajibu wao wa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani bila shuruti.
Akiongea na wadau hao, SSP Obonyo amewasihi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ili kubaini na kuzuia viashiria vyote vya uhalifu, huku akiwahimiza kutoa taarifa za siri pindi wanapobaini vitendo viovu vinavyotishia usalama wa wananchi na mali zao.
Kwa upande wao, waendesha bodaboda wamempongeza kamanda huyo na kuiomba polisi kuendelea kuwa karibu yao kwa kuwapatia elimu ya mara kwa mara ya usalama barabarani, jambo litakalowajengea uelewa mpana wa kujilinda na kuepuka hatua za kisheria zinazoweza kuepukika.
Naye mwakilishi wa mawakala wa mabasi katika stendi hiyo, Gosgen Makundi, amesema ushirikiano uliopo baina ya wananchi na jeshi la polisi umezidi kuimarika siku hadi siku, akisisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano huo ili kulinda amani na utulivu wa wilaya hiyo.

