NA DENIS MLOWE, IRINGA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesisitiza usimamizi madhubuti wa fedha za umma zinazotolewa kwa ajili ya kuboresha elimu ya juu nchini, akitaka kila shilingi iliyotengwa itumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukamilisha miradi kwa wakati na kuwanufaisha wanafunzi pamoja na jamii.
Ndejembi alitoa msisitizo huo mkoani Iringa wakati wa hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi saba ya miundombinu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), akisema uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo unapaswa kuendana na matumizi sahihi ya fedha na matokeo yanayoonekana.
Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa, Serikali imeelekeza zaidi ya Shilingi bilioni 175 mkoani Iringa kwa ajili ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari, huku ikiendelea kuwekeza katika elimu ya juu ili kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vikuu.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeelekeza zaidi ya dola milioni 425, sawa na takribani Shilingi trilioni moja kulingana na maelezo yaliyotolewa, kwa ajili ya kuboresha elimu ya juu nchini.
Alisisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, utafiti na huduma kwa wanafunzi huku ikihimiza uongozi wa chuo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na ndani ya muda uliopangwa.
Alisema Serikali inatarajia kuona majengo hayo yakianza kutumika na kuchangia kuboresha utoaji wa elimu ya juu nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alisema Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha walimu na wataalamu wanaohitajika katika maendeleo ya taifa tangu kilipoanzishwa mwaka 2005.
Alieleza kuwa chuo hicho kimezalisha wahitimu zaidi ya 19,000, huku miradi mipya ikitarajiwa kuongeza uwezo wa kutoa huduma za elimu, utafiti na malazi kwa wanafunzi.
Kikwete alisema pamoja na uwekezaji unaofanyika, bado kuna mahitaji muhimu yanayopaswa kushughulikiwa, yakiwemo kukamilisha ujenzi wa ghorofa ya tatu ya hosteli za wanafunzi, upatikanaji wa vifaa kwa wakati na ujenzi wa shule ya mazoezi ya chuo.
Alisema kukamilika kwa hosteli hizo kutasaidia zaidi ya wanafunzi 900 ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya kupata malazi ndani ya mazingira ya chuo.
Akijibu baadhi ya changamoto hizo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema Serikali imekubaliana na Katibu Mkuu wa wizara husika kuwa Shule ya Msingi Ilala iliyopo katika eneo la chuo ikabidhiwe kwa chuo hicho, huku taratibu za kiutawala zikiendelea kukamilishwa.




