Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

Oktoba 16,2026

WAZIRI Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba, amekataza kuwachangisha wananchi fedha za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa wanaopelekwa hospitali za rufaa, akisisitiza kuwa mamlaka zinazoyasimamia zinapaswa kuhakikisha yana mafuta na yanatoa huduma iliyokusudiwa.

Pia, amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutokuzuia miili ya marehemu hospitalini kutokana na madai ya malipo. 

Mwigulu ametoa katazo hilo oktoba 16,2026 wilayani Bagamoyo baada ya kupatiwa malalamiko yanayohusu wananchi kukerwa na kero hiyo katika hospital ya wilaya.

Amevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia ununuzi, usambazaji na matumizi ya dawa za serikali ili kuhakikisha zinawafikia wananchi.

Waziri Mkuu ameeleza sekta binafsi imara na viwanda vya kuchakata mazao ni muhimu katika kuongeza ajira na kipato. 

Amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji na uzalishaji, huku akisisitiza matumizi bora ya ardhi na uzingatiaji wa sheria.