
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Maktaba jijini Dar es Salaam Oktoba 16, 2026.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania (TCAF), CPA Nyakaho Mturi Mahemba akitoa maelezo ya mfuko huo namna unavyosaidia na kufanikisha masuala ya sanaa na utamaduni.
……………..
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda, amewataka waandishi na wachapishaji wa vitabu kuendelea kuandaa machapisho yanayokidhi mahitaji ya sasa ya jamii, yakiwemo vitabu vya watoto, vitabu vya rejea, kamusi na machapisho yanayohifadhi historia na utamaduni wa Tanzania.
Amesema vitabu vina mchango mkubwa katika kuendeleza elimu, kuhifadhi maarifa na kukuza sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo utalii, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha uchapishaji na usomaji ili tasnia hiyo iweze kukua na kushindana kimataifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vilivyowezeshwa kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Ntonda amesema vitabu ni nyenzo muhimu katika kuitangaza Tanzania kwa wageni na wananchi, kwa kutoa maarifa kuhusu historia, utamaduni na rasilimali za utalii zilizopo nchini.
Amesema kamusi zina nafasi ya pekee katika kukuza Kiswahili, kuimarisha mawasiliano, kuhifadhi msamiati na kurahisisha upatikanaji wa maarifa katika elimu, sayansi, teknolojia, biashara, diplomasia na maeneo mengine ya maendeleo.
Ntonda amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa wanafunzi na vijana wa vyuo, akieleza kuwa juhudi za waandishi na wachapishaji zinapaswa kwenda sambamba na hamasa kwa jamii kutumia vitabu kujielimisha na kuongeza ujuzi.
Ameahidi kuwa wizara itayafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa na wadau wa uchapishaji wa vitabu, kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika, huku akihimiza kuwepo kwa mikakati ya kuendeleza maonyesho ya vitabu na kuongeza ushiriki wa wadau ili kukuza tasnia hiyo nchini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania (TCAF), CPA Nyakaho Mturi Mahemba, amesema mfuko huo umeanzishwa kwa lengo la kuinua ubora wa kazi za utamaduni na sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara, kuzalisha ajira na kuchangia katika pato la Taifa.
Amesema mfuko huo unahudumia maeneo mbalimbali ya sanaa, yakiwemo sanaa za maonyesho, sanaa za ufundi, filamu na muziki, pamoja na maeneo ya lugha na fasihi katika sekta ya utamaduni.
Mahemba amesema eneo la lugha na fasihi linajumuisha uandishi wa makala na miswada, utunzi wa vitabu, mashairi na ngonjera, pamoja na uchapishaji, hivyo kuwa na mchango muhimu katika kukuza ubunifu na kuendeleza maarifa kupitia maandishi.
Amesema fasihi andishi ni nyenzo muhimu ya kuwasilisha mawazo, hisia, maarifa na uzoefu wa binadamu, huku ikisaidia kuhifadhi historia, mila, desturi, maadili na tamaduni za jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ameeleza kuwa uandishi pia hutumika kuelimisha, kuburudisha, kukosoa maovu na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii, hivyo kuifanya fasihi andishi kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya lugha na jamii kwa ujumla.
Mahemba amesema fasihi andishi inachangia maendeleo ya sanaa nyingine kwa kuwa maandishi hutumika kama msingi wa utengenezaji wa filamu na tamthilia kupitia miswada, pamoja na kusaidia ubunifu katika muziki na sanaa za maonyesho.
Amesema mchango huo unaifanya tasnia ya uandishi kuwa chanzo cha ubunifu, ajira na fursa za kiuchumi kwa wadau wa sekta mbalimbali, huku uwekezaji katika vitabu na machapisho ukiendelea kufungua nafasi za maendeleo kwa waandishi na wachapishaji.
Amebainisha kuwa mfuko huo umewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Sh2,364,198,270.08 kwa miradi 104 katika eneo la lugha na fasihi, hatua inayolenga kuimarisha shughuli za wadau wanaojishughulisha na uandishi na uchapishaji.
Amesema mikopo hiyo imesaidia ununuzi wa mashine za uchapishaji, kuboresha miundombinu ya maduka ya vitabu na kuchapisha nakala zinazotumika mashuleni, maofisini, vyuoni na hotelini, hatua inayosaidia kupanua upatikanaji wa vitabu katika maeneo mbalimbali.
Mahemba amewahimiza wadau kuendelea kuithamini fasihi andishi kwa kuwekeza katika uandishi, kuimarisha usomaji, kukuza uchapishaji na kujenga ushirikiano kati ya fasihi andishi na sanaa nyingine, akisema hatua hizo zitasaidia kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kufungua fursa mpya kwa vizazi vijavyo.

