Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya kimataifa ya kulinda bioanuai lazima iambatane na hatua halisi zinazohakikisha mifumo ya ikolojia inalindwa, inarejeshwa na kutumiwa kwa njia endelevu kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya uchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 16 Oktoba 2026, mjini Yerevan, Armenia, wakati akihutubia Mkutano wa Viongozi kuhusu Bioanuai (Leaders’ Summit on Biodiversity), akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tanzania imeweka mwelekeo wa utekelezaji kupitia Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Bioanuai wa 2025–2030, unaolenga kuimarisha uhifadhi, kurejesha mifumo ya ikolojia na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Akieleza hatua za Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema hifadhi za bahari zimeongezeka kutoka tano hadi saba, huku eneo la uhifadhi likiongezeka kutoka takriban kilomita za mraba 2,400 hadi zaidi ya 3,600, ikiwemo maeneo mawili mapya ya Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa uhifadhi wa bioanuai lazima ulete manufaa kwa jamii, huku wananchi wakishirikishwa katika uhifadhi, urejeshaji na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Amesema lengo la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya ardhi na bahari ifikapo mwaka 2030 linahitaji usimamizi bora, fedha, teknolojia na ushiriki wa jamii. Tanzania pia inatarajia kupitishwa kwa Wito wa Yerevan wa Kuchukua Hatua (Yerevan Call for Action), tamko la kisiasa linalolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo ya bioanuai kuelekea mwaka 2030.
Pembezoni mwa mkutano huo, Rais Dkt. Mwinyi ameshiriki Kikao cha Majadiliano ya Ngazi ya Juu kuhusu Ufadhili wa Bioanuai na Uwekezaji unaozingatia mazingira, kilichohudhuriwa na Rais wa Armenia pamoja na viongozi kutoka nchi mbalimbali, ambapo wamejadili namna ya kuimarisha ufadhili, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha za kimataifa na sekta binafsi katika kulinda na kurejesha bioanuai.
Katika majadiliano hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania inaendelea kuweka kipaumbele katika kuongeza rasilimali za kifedha kwa ajili ya uhifadhi wa bioanuai, sambamba na kuhakikisha sera za uwekezaji na uchumi zinachangia maendeleo yanayolinda mazingira. Amesema Tanzania inalenga kupata takriban dola za Marekani milioni 41 kupitia mifumo ya kimataifa ya ufadhili wa mazingira ili kutekeleza miradi ya uhifadhi na urejeshaji wa mifumo ya ikolojia.
Mkutano huo umehudhuriwa na Marais wa nchi mbalimbali, Mawaziri Wakuu, Wakuu wa Ujumbe na viongozi wa mashirika ya kimataifa kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Rais Dkt. Mwinyi ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya, Balozi wa Tanzania nchini Urusi anayewakilisha pia Armenia, Mhe. Fredrick Ibrahim Kibuta, pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali wa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Armenia na kuondoka leo, tarehe 16 Oktoba 2026, baada ya kushiriki Mkutano wa Viongozi kuhusu Bioanuai (Leaders’ Summit on Biodiversity) mjini Yerevan, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

