Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, kwa kushirikiana na Axium Collective, umeandaa hafla ya chakula cha mchana na majadiliano ya utalii tarehe 16 Oktoba 2026, jijini Paris, ikiwa ni hitimisho la Tanzania Leaders Club Roadshow 2026.

Hafla hiyo, iliyoongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, imewakutanisha wawakilishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Qatar Airways, Tanganyika na kampuni nyingine za utalii na hoteli. Pia imehudhuriwa na waandaaji wa safari na waandishi wa habari za utalii nchini Ufaransa, pamoja na baadhi ya washiriki kutoka Uholanzi, Ubelgiji na Luxembourg.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Yakubu ameeleza kuwa juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimeendelea kuimarisha utangazaji wa vivutio vya Tanzania kimataifa, ikiwemo kupitia filamu ya Tanzania: The Royal Tour.

Amehimiza kuendelezwa kwa juhudi hizo kupitia kampeni za kidijitali kwa lugha ya Kifaransa, safari za utambulisho kwa waandishi wa habari na waandaaji wa safari, pamoja na kuimarisha ushirikiano na mashirika ya ndege ili kuongeza watalii kutoka Ufaransa na masoko mengine ya Ulaya.

Aidha, amewahamasisha wadau kuandaa vifurushi vinavyounganisha vivutio mbalimbali vya Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuwapa wageni uzoefu mpana, kuongeza muda wa kukaa nchini na kupanua manufaa ya utalii kwa wananchi.

Balozi Yakubu ameishukuru Axium Collective, taasisi na kampuni zilizoshiriki pamoja na wadhamini kwa kufanikisha roadshow hiyo, akisisitiza umuhimu wa kugeuza mawasiliano yaliyojengwa kuwa ushirikiano wa kudumu na ongezeko la safari za watalii kwenda Tanzania.